1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi 14, Ujerumani ikiwemo, zajiunga na Baraza la Haki la UN

Daniel Gakuba
12 Oktoba 2022

Ujerumani imerejea katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, baada ya kuchaguliwa katika Baraza Kuu la umoja huo jana jioni. Nchi nne za Afrika; Sudan, Algeria, Moroko na Afrika Kusini pia zimechaguliwa.

https://p.dw.com/p/4I3zU
Schweiz Genf | Sitzung UN-Menschenrechtsrat
Picha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Kura hiyo ya siri ilipigwa kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lenye nchi wanachama 193, kujaza nafasi 14 kwenye Baraza la Haki za Binadamu lenye viti 47. Ujerumani imepita kwa kupata kura 167 katika ya 176 zinazowezekana, ikiwa na maana kuwa itakaa katika baraza hilo kwa miaka mitatu, kuanzia 2023 hadi 2025.

Soma zaidi: UNHCR yakataa kufanyika kwa mjadala wa Xinjiang

Nchi nyingine zilizofanikiwa kuchaguliwa katika baraza hilo ni Algeria, Bangladesh, Ubelgiji, Chile, Costa Rica na Georgia. Nyingine ni  Kyrgyzstan, Maldives, Moroko, Romania, Afrika Kusini, Sudan na Vietnam.

Venezuela, Korea Kusini na Afghanistan pia zilijaribu lakini zilishindwa kupata kura za kutosha kuziunga mkono.

Mtindo wa uchaguzi unaoleta utata

Viti katika baraza hilo husambazwa katika utaratibu unaohakikisha kuwa kanda zote za dunia zinawakilishwa. Makundi ya kutetea haki za binadamu yanaukosoa mtindo huo, kwa hoja kwamba unazinyima nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa chaguo huru la nchi zifaazo, na kuzihakikishia nafasi baadhi ya nchi zenye rekodi mbaya ya haki za binadamu.

Großbritannien London | Protest gegen Menschenrechtsverletzungen in China
Muundo wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa huamua mijadala na maamuzi ya baraza hiloPicha: Alexander Mak/NurPhoto/picture alliance

Mwaka huu kinyang'anyiro kilichofuatiliwa kwa karibu ni kile cha ukanda wa Amerika Kusini na Karibeani, ambako Chile, Costa Rica na Venezuela ziliwania viti viwili. Viti hivyo vimenyakuliwa na Chile pamoja na Costa Rica, huku Venezuela ikitubwa nje kwa kuambulia kura 88.

Soma zaidi: Bachelet aataka haki za wanawake ziheshimiwe Afghanistan

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Louis Charbonneau amekaribisha kushindwa kwa Venezuela, akisema wachunguzi wa Umoja wa Mataifa walipata ushahidi kuwa rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro na maafisa wengine wa serikali yake, wanawajibika katika uhalifu dhidi ya ubinadamu waliotendewa raia wa Venezuela.

Mabadiliko yatarajiwa katika maamuzi ya baraza

Wachambuzi wa mambo wanasema uchaguzi huu wa jana ni muhimu kwa sababu utabadilisha wizani wa maoni katika baraza la haki za binadamu lenye migawanyiko mikubwa. Matokeo ya kura katika baraza hilo lenye makao yake mjini Geneva yamekuwa ya kukaribiana sana hivi karibuni, mfano ukiwa wiki iliyopita ambapo upande unaoongozwa na nchi za magharibi ulishindwa kwa kura mbili tu, kuitisha mdahalo juu ya tuhuma dhidi ya China za uvunjifu wa haki za binadamu katika jimbo la Xinjiang.

 

Vyanzo:ape, dpae