1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRomania

NATO yajitolea kwa uanachama wa baadaye wa Ukraine

29 Novemba 2022

Katibu mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg, amesisitiza kujitolea kwa muungano huo wa kijeshi kwa Ukraine na kusema taifa hilo lililoghubikwa na vita siku moja litakuwa mwanachama wake.

https://p.dw.com/p/4KFGW
NATO Secretary-General Jens Stoltenberg speaks to DW
Picha: DW

Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili, Stoltenberg amesema kuwa mlango wa NATO uko wazi na kwamba Urusi haina kura ya turufu kwa nchi kujiunga na jumuiya hiyo akimaanisha hatua ya hivi karibuni ya Macedonia na Montenegro Kaskazini kujiunga na muungano huo wa kijeshi.

Stoltenberg amesema kuwa rais wa Urusi Vladimir Putin, hivi karibuni atazipata Finland na Sweden kama wanachama wa NATO. Mataifa hayo majirani ya Nordic yaliomba uanachama katika jumuiya ya NATO mnamo mwezi Aprili yakiwa na wasiwasi kwamba huenda Urusi ikayalenga.

Stoltenberg asema mamilioni ya wakimbizi wa Ukraine waingia Romania

Kimsingi, Stoltenberg alirudia kiapo kilichotolewa na viongozi wa NATO mjini Bucharest mnamo 2008 katika  bunge hilo  ambapo mawaziri wa mambo ya nje wanakutana wiki hii kwamba Ukraine, na pia Georgia, siku moja zitajiunga na muungano huo.

Soma pia: Mawaziri wa NATO wakutana kujadili kadhia ya vita Ukraine

Stoltenberg ameongeza kusema kwamba wameona mamilioni ya watu wakilazimika kukimbia Ukraine na kwamba tayari wengi wao wamevuka mpaka na kuingia Romania, karibu milioni 3. Ameendelea kusema kwamba hali hiyo inaonesha jinsi ilivyo kwa wakati na muhimu kwamba wakutane katika mpaka wa Romania na Ukraine. 

 Stoltenberg amesema kuwa Urusi inashindwa katika uwanja wa vita, na kutokana na hilo, sasa imeanza kushambulia malengo ya raia na miji.

Russland Moskau | Präsident Wladimir Putin
Rais wa Urusi - Vladimir PutinPicha: Pavel Bednyakov/POOL/TASS/dpa/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza James Cleverly amesema kuwa ulengaji huo wa miundombinu ya kiraia na nishati ni dhahiri kwamba kunajaribu kuwashinikiza raia wa Ukraine kusalimu amri, jambo ambalo anafikiria haliwezi kufanikiwa.

Ukraine yaomba ulinzi zaidi wa anga

Mataifa washirika wameipa Ukraine silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola, lakini Ukraine inaomba ulinzi zaidi wa anga, magari ya vita na makombora ya masafa marefu ili kuvirudisha nyuma vikosi vya Urusi. Lakini kuna wasiwasi kwamba hifadhi za silaha katika baadhi ya mataifa ya NATO zinaendelea kupungua kwa kuwa silaha nyingi zimepelekwa Ukraine.

Soma pia: Ukraine imesema Urusi inajiandaa na mashambulizi mapya

Waziri wa mambo ya nje wa Lithuania Gabrielius Landsbergis amesema ombi lake kwa mawaziri wenza wa NATO ni rahisi: kutulia na kutoa magari ya vita. 

Ujerumani ambayo kwasasa inashikilia uenyekiti wa kundi la nchi saba zilizostawi kiviwanda G7, imeandaa mkutano leo mchana pembezoni mwa mkutano huo wa NATO kuzungumzia mzozo huo wa nishati uliosababishwa na Ukraine. Kulingana na maafisa wa Marekani, taifa hilo litatoa wito kwa mataifa wanachama kuimarisha msaada wao katika sekta hiyo.