1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine imesema Urusi inajiandaa na mashambulizi mapya

28 Novemba 2022

Ukraine imesema leo kuwa Urusi inajiandaa kwa wimbi jipya la mashambulizi ya makombora kwenye miundombinu yake ya nishati ambayo yameitumbukiza nchi hiyo kwenye baridi na giza.

https://p.dw.com/p/4KBxo
Ukraine-Krieg - Kiew
Picha: Patrice Bergeron/Canadian Press via ZUMA Press/picture alliance

Msemaji wa jeshi la Ukraine Natalia Gumeniuk amesema kuwa meli ya kivita ya Urusi yenye uwezo wa kurusha makombora ya masafa marefu ilitumwa hivi karibuni kwenye Bahari Nyeusi ikiwa na makombora aina ya Kalibr, na kwamba hii inaashiria kuwa maandalizi ya mashambulizi yalikuwa yanaendelea.

Huku hali ya baridi ikizidi kuwa kali, mashambulizi ya mara kwa mara ya Urusi katika wiki za hivi karibuni, yameharibu miundombinu ya nishati ya Ukraine na hivyo kutatiza usambazaji wa umeme na maji kwa mamilioni ya watu.

Ukraine | Oleksiy Kuleba während Interview in Kiew
Gavana wa mkoa wa Kyiv Oleksiy KulebaPicha: VALENTYN OGIRENKO/REUTERS

Katika mkururo wa hivi majuzi wa makumi ya mashambulizi ya Urusi kuelekea Ukraine, Gavana wa mkoa wa  Kyiv Oleksiy Kuleba amesema leo kuwa wakaazi wa ndani na karibu na mji mkuu huo, bado walikuwa wakikabiliwa na usumbufu wa uhaba wa maji na umeme kutokana na mashambulizi ya Urusi huku karibu asilimia 40 ya kaya zikiwa bado hazina umeme.

Soma zaidi:Umeme warejea kwenye maeneo karibu yote ya Kiev 

Katika hotuba yake kwa raia wa Ukraine usiku wa kuamkia leo, Rais Volodymyr Zelenskyy alitahadharisha kwamba Urusi ilikuwa ikitayarisha mashambulizi mapya ya angani na kusema vikosi vya Moscow vitaendeleza mashambulizi kwa kipindi chote watakapokuwa na makombora.

Der ukrainische Präsident Wolodymyr Selenskji
Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyyPicha: Spencer Platt/AFP/Getty Images

Zelenskyy ameongeza kuwa jeshi la Ukraine limejiandaa kwa ushirikiano na washirika wa Magharibi, ambao wamekuwa wakiwasilisha mifumo mipya ya ulinzi wa anga kwa Ukraine. Ofisi ya rais wa Ukraine imesema leo kwamba mashambulizi ya Urusi yamesababisha jana vifo vya watu wanne katika maeneo kadhaa yanayokumbwa na vita.

Soma zaidi: Shambulio dhidi ya hospitali ya wazazi laua kichanga Ukraine

Urusi yasema Ukraine haitaki mazungumzo

Urusi kwa upande wake imesema inalenga tu miundombinu yenye mafungamano na jeshi na kwamba kukatika kwa umeme na athari zake kwa raia, hakusababishwi na mashambulio yake ya makombora bali kunatokana na Ukraine kukataa kufanya mazungumzo na Moscow.

Der russische Pressesprecher Dmitry Peskov
Msemaji wa Ikulu ya Urusi, (Kremlin), Dmitry Peskov Picha: Elena Palm/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Kremlin Dmitry Peskov amesema:

"Tunafahamu kwamba idadi ya viongozi na nchi kadhaa za kigeni wamekuwa wakitangaza utayari wao wa kutoa jukwaa la upatanishi, na kwa hakika tumepokea vyema utashi huo wa kisiasa. Urusi imepokea vyema pendekezo la Vatican la kutoa jukwaa la mazungumzo ili kuutatua mzozo wetu na Ukraine, lakini msimamo wa sasa wa Kyiv unafanya juhudi za upatanishi kutowezekana."

Soma zaidi:Raia wa Ukraine wanateseka kwa baridi, huku rais akiomba Umoja wa Mataifa kuiadhibu Urusi 

Bahrain | Rückreise Papst Franziskus
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa FrancisPicha: Maurizio Brambatti/AP Photo/picture alliance

Siku 10 zilizopita, akiwa katika mahojiano na Jarida la kila siku la Italia "La Stampa", Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis  alisema Vatican ilikuwa tayari kufanya kila linalowezekana ili kupatanisha na kusitisha mgogoro kati ya Urusi na Ukraine.

Wakati huohuo Wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon imesema itazingatia pendekezo la kuipatia Ukraine makombora zaidi na yenye ufanisi ambayo yatairuhusu Kyiv kupambana na vikosi vya Urusi wakati Mataifa ya Magharibi yakijitahidi kukidhi mahitaji ya silaha zaidi kwa taifa hilo.