NATO yaanza mazoezi makubwa ya kijeshi kuonyesha nguvu zake
12 Juni 2023Mazoezi hayo makubwa ya kijeshi yaliyopewa jina la "Air Defender 23", yanayofanyika katika anga ya Ujerumani na yanayoongozwa na taifa hilo lililo na uchumi mkubwa barani Ulaya, yanaanza leo tarehe 12 hadi tarehe 23 Juni na yatajumuisha ndege 250 za kijeshi, kutoka nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Kujihami NATO pamoja na nchi washirika kama Japan na Sweden zilizoomba kujiunga na Jumuiya hiyo.
Wanajeshi zaidi ya 10,000 watajiunga katika mazoezi hayo yaliyo na nia ya kuimarisha mshikamano na utayarifu wa kujilinda dhidi ya ndege za kivita zisizokuwa na rubani, pamoja na makombora, wakati patakapotokea shambulio mijini, katika viwanja vya ndege na baharini karibu na maeneo ya NATO.
Wanajeshi wa nchi wanachama NATO watapokea mafunzo katika anga tatu za Ujerumani, kwenye bahari ya kaskazini, eneo la mashariki mwa Ujerumani na katika ukanda mdogo wa kusini mwa Ujerumani.
NATO kufanya luteka kubwa ya angani nchini Ujerumani
Wiki iliyopita Luteni jenerali Ingo Gerhartz, Kamanda wa jeshi la anga la Ujerumani, alisema mpango wa "Air Defender" ulianzishwa mwaka 2018 kama jibu dhidi ya hatua ya Urusi ya kunyakuwa eneo la Crimea kutoka kwa jirani yake Ukraine miaka minne iliyopita, lakini akasisitiza kuwa hawamlengi mtu yeyote.
Alisema anachojua ni kwamba NATO itaendelea kutetea eneo lake lote inalolidhibiti na kwamba zoezi hilo halitatuma ndege zozote Kaliningrad, ambalo ni eneo la Urusi linalopakana na wanachama wa NATO Poland na Lithuania.
Macron, Scholz na Duda waijadili Ukraine mjini Paris
Huku hayo yakiarifiwa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atakutana hii leo mjini Paris na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani na rais wa Poland Andrzej Duda in kujadili hatua zaidi za kuisaidia Ukraine pamoja na matayarisho ya mkutano wa kilele wa NATO unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Zelensky asema operesheni ya kujibu mashambulizi ya Urusi inaendelea
Mazungumzo yao yatatuwama juu ya usaidizi wa kijeshi kwa Ukraine ili kukabiliana na uvamizi wa Urusi pamoja na msaada wa kiutu hasa katika eneo la Kherson. Watajadili pia kuhusu usalama wa muda mrefu kwa Ukraine ili kulinda uhuru wa taifa hilo pamoja na maeneo yake.
Kwa muda mrefu sasa Ukraine imekuwa ikiomba kujiunga na Jumuiya ya NATO. Japo washirika wakubwa wa NATO wamekuwa na wasiwasi kufuatia ombi hilo, mazungumzo yanaendelea ya kuibadili kamisheni ya NATO-Ukraine kuwa Baraza la NATO Ukraine kuwa jukwaa la pamoja litakalojadili masuala ya usalama na Kiev.
Ujerumani na Marekani hawajaonyesha nia kamili ya kukubali ombi la Ukraine kwa kuhofia jibu litakalotoka Urusi iwapo hilo litafanyika.
Chanzo: afp/dpa