1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO ni nini na kwanini iliundwa?

8 Februari 2022

Wakati kukiwa na mzozo juu ya NATO kutanua uwepo wake mashariki mwa Ulaya na ubabe wa Urusi dhidi ya Ukraine, DW inaangazia chimbuko na malengo ya muungano huo wa kijeshi wa mataifa ya Ulaya na Marekani.

https://p.dw.com/p/46hPO
Bundeswehrsoldaten in Litauen
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Jumuiya ya kujihami ya mataifa ya magharibi, NATO, iliundwa mnamo mwaka 1949 ikiwa na lengo, kwanza kabisa la kuwa kama kizuizi dhidi ya kitisho cha upanuzi wa Jamhuri ya Kisovieti barani Ulaya baada ya Vita Vikuu vya pili vya Dunia.

Zaidi ya hapo, Marekani iliiona jumuiya hiyo kama zana ya kuzuia kuibuka tena kwa hisia za uzalendo barani Ulaya na kukuza ushirikishwaji wa kisiasa barani humo.

Soma pia: Stoltenberg asema NATO haina mpango wa kuwapeleka wanajeshi Ukraine

Chimbuko lake, hata hivyo, linakwenda nyuma kwenye mwaka wa 1947, wakati Uingereza na Ufaransa ziliposaini mkataba  wa Dunkirk kama muungano wa kukabiliana na uwezekano wa shambulio la Ujerumani baada ya kumalizika kwa vita.

Mataifa wanachama 12 ya awali yaliyoasisi muungano huo wa kisiasa na kijeshi ni Marekani, Uingereza, Ubelgiji, Canada, Denmark, Ufaransa, Iceland, Italia, Luxembourg, Uholanzi, Norway na Ureno.

Brüssel NATO Gipfeltreffen l Generalsekretär Stoltenberg
Picha: Kenzo Tribouillard/AFP

Jumuiya hiyo hutumiwa kama muungano wa usalama wa pamoja wenye  lengo la kutoa ulinzi kwa pande zote kwa njia za kijeshi na kisiasa ikiwa moja ya nchi mwanachama inatishiwa na nchi nyingine ya nje ya muungano.

Msingi wake umeainishwa katika kifungu cha 5 cha mkataba wa kuasisiwa kinachozungumzia ulinzi wa pamoja.

Soma pia: Putin asema Marekani na NATO zimepuuza matakwa ya Urusi

Kifungu cha 5 kimewahi kutumiwa mara moja na Marekani baada ya , shambulio la Septemba kumina moja 9/11 mnamo mwaka  2001.

Umoja wa Kisovieti ulijibu hatua ya  NATO kwa kuunda muungano wake wa kijeshi na mataifa mengine saba ya kikomunisti ya Ulaya Mashariki mnamo mwaka 1955, uliyopewa jina la Mkataba wa Warsaw.

Utaratibu mpya wa usalama Ulaya

Lakini kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, na kuvunjika  kwa Muungano wa Kisovieti mwaka 1991, kulifungua njia ya utaratibu mpya wa usalama wa baada ya Vita Baridi barani Ulaya.

Baada ya kupata uhuru wake kutoka  Jamhuri ya Kisovieti, nchi kadhaa za zamani za Mkataba wa Warsaw zilijiunga na Jumuiya ya NATO.

Infografik NATO Osterweiterung EN v2
Idadi ya mataifa wanachama wa NATO na miaka yao ya kujiunga.

Wanachama wa kundi la  Visegrad, ambazo ni  Hungary, Poland na Jamhuri ya Cheki zilijiunga mwaka 1999.

Miaka mitano baadaye, NATO iliidhinisha kujiunga kwa kile kinachoitwa kundi la Vilnius, lililoundwa na mataifa ya Bulgaria, Estonia, Latvia, Lithuania, Romania, Slovakia na Slovenia. Albania na Croatia zilijiunga mwaka wa 2009.

Soma pia: Urusi: Majibu ya Marekani kuhusu Ukraine hayaridhishi

Nchi za karibuni zaidi kujiunga na muungano huo ni Montenegro mwaka 2017 na Macedonia Kaskazini  iliyojiunga mwaka 2020, na kufanya jumla ya idadi ya nchi wanachama kufikia 30.

Nchi tatu kwa sasa zimeainishwa kama "wanachama wanaozingatiwa" ambazo ni Bosnia-Herzegovina, Georgia na Ukraine.

Kutokana na mzozo wa sasa  kati ya Urusi na Ukraine kwenye mpaka wao wa pamoja, shauku ya nchi hiyo kujiunga na NATO imeshika tena  kasi.

Katika mkutano wa kilele wa NATO uliofanyika  Bucharest mwaka 2008, muungano huo ulikaribisha rasmi matarajio ya uanachama wa Ukraine na Georgia, lakini ulisita kutoa mipango ya utekelezaji kuwapa uanachama. Kwa Urusi, hata hivyo, wazo la Ukraine kujiunga na NATO ni mstari mwekundu.

Chanzo: DW