1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi: Majibu ya Marekani kuhusu Ukraine hayaridhishi

Daniel Gakuba
27 Januari 2022

Ikulu ya Kremlin mjini Moscow imesema hatua ya Marekani kupuuza matakwa makuu ya kiusalama ya Urusi inadhoofisha matumaini ya suluhisho la amani kwa mzozo wa Ukraine, na kuongeza lakini kuwa bado mazungumzo yanawezekana

https://p.dw.com/p/46By8
Russland | Kreml-Sprecher Dmitri Peskow
Msemaji wa Ikulu ya Urusi - Kremlin, Dmitry PeskovPicha: Shamil Zhumatov/AFP/Getty Images

Kauli hiyo ya ofisi ya rais wa Urusi imefuatia tangazo la Marekani, kwamba imeyajibu kwa maandishi madai yaliyowasilishwa na Urusi, ya kutaka ihakikishiwe kuwa kamwe Ukraine haitakaribishwa kama mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO, na kwamba jumuiya hiyo haitajitanua zaidi upande wa mashariki.

Soma pia: Marekani, NATO watoa jibu la maandishi kwa masharti ya Urusi

Marekani imesema katika majibu yake yaliyoihusisha NATO, kuwa imekataa kuridhia matakwa hayo ya Urusi. Msemaji wa Ikulu ya Urusi Dmitry Peskov, amesema Rais Vladimir Putin atashauriana na wasaidizi wake juu ya jibu hilo la Marekani na NATO.

''Rais anashauriana na maafisa wake pamoja na baraza lake la usalama. Siwezi kubashiri jibu litakuja lini lakini halitachelewa sana. Itakuwa ujinga kufikiri kuwa litakuja kesho, kwa sababu, tusisahau kuwa iliichukua Marekani na Ulaya nzima zaidi ya mwezi mmoja kuzisoma na kuzitafakari nyaraka zetu.''

Militärübung in Russland
Jeshi la Urusi limejikusanya kwenye mpaka wa UkrainePicha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/dpa/picture alliance

Pamoja na hayo, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema kuwa jibu la Marekani na NATO, japo limepuuza madai muhimu zaidi, linatoa fursa ya kuyajadili baadhi ya masuala mengine madogo madogo.

Huku hayo yakijiri, Ujerumani ambayo imekabiliwa na ukosoaji kutoka washirika wake wa magharibi, imetetea uamuzi wake wa kukataa kuipatia Ukraine silaha za kivita za kupambana na Urusi.

Waziri wa Ujerumani wa mambo ya nje Annalena Baerbock amewaambia wabunge mjini Berlin kuwa serikali ya kansela Olaf Scholz inazingatia msemo kwamba, ''wakati wa mazungumzo, usifyatue risasi'', akisisitiza kuwa chochote kitakachofanywa na Ujerumani kitazingatia umuhimu wa kuacha wazi mlango wa mazungumzo.

Kwa upande wake, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema ameridhishwa na matokeo ya mazungumzo yaliyofanyika baina ya wawakilishi wa nchi yake na wa Urusi mjini Paris hapo jana, yakihusisha Ufaransa na Ujerumani. Kupitia tangazo la ofisi yake, rais huyo amesema yalikuwa yenye tija, ambayo yatafuatiwa na mengine mapana zaidi mjini Berlin katika muda wa wiki mbili zijazo.

Mzozo umeshamiri miezi ya hivi karibuni baina ya Urusi na nchi za magharibi, baada ya Urusi kurundika wanajeshi zaidi ya 100,000 karibu na mpaka wa Ukraine, kitendo ambacho nchi za magharibi zinashuku kitaishia katika kuivamia Ukraine. Urusi inazikanusha shutuma hizo, na leo hii imesema hata kuzungumzia vita baina yake na Ukraine ni kitu kisichokubalika.

ape,afpe, rtre