1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO imesema imewauwa waasi 40 zaidi wa Taliban nchini Afghanistan

9 Septemba 2006
https://p.dw.com/p/CDDx

Vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na jumuia ya kujihami ya magharibi NATO nchini Afghanistan vimesema vimewauwa wanamgambo 40 zaidi wa Taliban katika mapigano yanayoendelea kusini mwa nchi hiyo.Jumuia ya kujihami ya magharibi NATO imesema mapigano yanaendelea katika mkoa wa Kandahar.Waasi 300 wameuwawa tangu mapigano hayo yaliporipuka wiki moja iliyopita.Mapigano hayo yamejiri baada ya mtu aliyeyatolea mhanga maisha yake kujiripua mjini Kabul na kuwauwa watu 16-wakiwemo wanajeshi wawili wa kimarekani.Mapigano hayo yamesadif pia wakati majerenali wa kutoka nchi 26 za jumuia ya kujihami ya magharibi NATO wanakutana nchini Poland kuzungumzia namna ya kuimarisha shughuli za vikosi vya NATO nchini Afghanistan.Katika mkutano huo wa siku mbili majenerali wanapendekeza wanajeshi 2000 zaidi wapelekwe Afghanistan ambako NATO inakumbana na mashambulio yasiyokwisha kusini mwa nchi hiyo.Duru kutoka mjini Warsaw mji mkuu wa Poland zinasema nchi za NATO zinakubaliana kimsingi juu ya umuhimu wa kutumwa wanajeshi hao-Hata hivyo hakuna uamuzi timamu uliofikiwa.