1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiChina

China ilivyogeuka mkusanyaji mkubwa wa madeni duniani

27 Novemba 2023

China imetoa mikopo ya dola trilioni 1.3 kwa ajili ya miradi ya miundombinu kuanzia Asia hadi Amerika Kusini ili kukuza biashara. DW inauliza jinsi China itakavyohakikisha madeni hayo yanalipwa.

https://p.dw.com/p/4ZV4K
Uongozi | Rais wa China Xi Jinping
Rais wa China Xi JinpingPicha: Andy Wong/AP Photo/picture alliance

Mpango mkubwa wa China wa Ukanda wa Barabara na Reli, BRI - unaounga mkono na mara nyingi kujenga baadhi ya miradi 21,000 ya miundombinu duniani kote - unachukuliwa kuwa kitovu cha sera ya kigeni ya Rais Xi Jinping.

Mara kwa mara ikilinganishwa na mpango wa usaidizi wa Marekani kwa Ulaya baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Beijing imejipatia zaidi ya dola trilioni 1.3 kutokana na mikopo yake katika kipindi cha muongo mmoja uliopita. Mikopo hiyo ikiwa ya kufadhili ujenzi wa madaraja, bandari na Barabara katika nchi zenye mapato ya chini au ya kadri, kulingana na ripoti mpya.

Mpango wa China wa BRI umesaidia kurejesha njia za zamani za biashara kati ya China na ulimwengu wote, thibitisho la jina lake la utani ‘Barabara Mpya ya Hariri'. Pia imeongeza ushawishi wa kimataifa wa Beijing, kiasi cha kuzighadhabisha Washington na Brussels.

Soma pia:China yaionya Korea Kusini kutoingiza siasa kwenye uchumi

Wakosoaji wanasema mpango wa BRI umeziacha nchi masikini na madeni makubwa na kuacha alama kubwa ya kaboni wakati ambapo ulinzi wa mazingira unapaswa kupewa kipaumbele. Baadhi ya nchi, ikiwemo Ufilipino, zimejiondoa katika miradi hiyo.

Wengine wameelezea mkakati wa China kuzipa kampuni zinazomilikiwa na serikali yake kandarasi au mikataba ya kujenga miundo mbinu ambayo gharama ya ujenzi aghalabu huwa ghali na nchi hutatizika kujadili upya mikataba hiyo baadaye.

Ingawa China imejitolea kuendelea kuwekeza mabilioni ya fedha kwenye miradi mipya, siku ya majuto imewadia. Muda wa kulipa madeni ya mikopo hiyo ya miaka 10 iliyopita umewadia.

Je ni mikopo ipi ya BRI imekuwa balaa kulipwa?

Ripoti iliyotolewa wiki iliyopita na shirika la AidData inakadiria kuwa asilimia 80 ya mikopo iliyotolewa na China katika mataifa maskini inasababisha shida za kifedha katika nchi hizo.

Taasisi hiyo ya utafiti yenye makao yake makuu nchini Marekani ilikadiria kuwa jumla ya madeni ambayo hayajalipwa, bila kujumuisha riba, ni takriban dola trilioni 1.1.

Biden na Xi washinikiza ushirikiano katika mkutano wao Bali

Japo ripoti hiyo haiainishi ni idadi ya madeni ambayo hayajalipwa, imeeleza kuwa idadi ya madeni hayo inazidi kuongezeka

Watafiti wa ripotihiyo pia walibaini kuwa miradi 1, 693 ya BRI ipo katika hatari ya kutumbukia nyongo na miradi mingine 94 imefutwa au imeahirishwa.

Aidha shirika la AidData ilikadiria kuwa zaidi ya nusu ya mikopo chini ya mpango wa BRI, zimefikia muda wa malipo yao kuhitimishwa. Haya yanajiri mnamo wakati viwango vya riba vya kimataifa vimepanda kwa kasi, hivyo kupa mataifa yenye madeni, mzigo mkubwa zaidi wa ulipaji.

Watafiti wa ripoti hiyo waligundua kuwa katika baadhi ya matukio, China imeongeza zaidi ya maradufu kiwango cha riba kama adhabu ya kuchelewa kwa malipo kutoka asilimia 3 hadi asilimia 8.7.

Soma pia:Mkutano wa marais wa Marekani na China una maana gani kwa Ujerumani

Wakati China ilipoanza kuyapa mataifa maskini mikopo mwanzoni mwa karne hii, chini ya theluthi moja ya miradi iliwekewa dhamana, ikilinganishwa na sasa ambapo karibu theluthi mbili ya miradi imewekewa dhamana.

Mapema mwaka huu, ripoti ya benki ya Dunia iligundua kuwa Beijing tayari ililazimika kutoa mabilioni ya mikopo ya uokozi kwa mataifa ya BRI.

Kwa sasa China inatumia mkakati mpyakujiepusha dhidi ya wimbi la mikopo iliyoshindikana kulipwa. AidData iligundua kuwa miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na mikopo ya uokozi ambayo inasaidia kuimarisha fedha za serikali ambazo imezikopesha, hasa benki zao kuu.

Marekani na EU zinafanya nini kushindana na China?

AidData iligundua kuwa China hutumia takriban dola bilioni 80 kila mwaka kutoa mikopo kwa nchi masikini huku Marekani ikijaribu kuifuata.

Diplomasia | Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakiwa katika mkutano Ikulu ya Marekani
Rais wa Marekani Joe Biden na maafisa wa ngazi za juu wakiwa katika mkutano na viongozi wa Umoja wa Ulaya wakiongozwa na Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Washington hutumia takriban dola bilioni 60 kila mwaka kufadhili miradi sawa ya maendeleo. Ni kulingana na Shirika la Fedha la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (DFC).

Mwezi uliopita, Umoja wa Ulaya ulifanya mkutano wake wa kwanza wa kilele kuhusu mpango wake wa Global Gateway, ambao pia unaonekana kama mbadala wa BRI na unatarajiwa kusaidia kuimarisha ushawishi wa Ulaya, hasa katika ‚Kusini mwa Ulimwengu.‘

Soma pia:Marais wa Marekani Joe Bden, na wa China Xi Jinping kukutana pembezoni mwa kutano wa APEC

Katika mazungumzo ya mwisho, miradi yenye thamani ya takriban dola bilioni 70 ilisainiwa kati ya serikali mbalimbali za Ulaya, Asia na Afrika.

Usaidizi huo wa Umoja wa Ulaya ambao hatimaye unaweza kufikia Euro bilioni 300, utasaidia miradi inayohusiana na madini ghafi muhimu, nishati salama na njia za usafiri.