1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Ukraine: Juhudi za kidiplomasia zaendelea

18 Februari 2022

Urusi imesema inaendelea kuviondoa vifaru na magari mengine ya kivita kutoka kwenye maeneo ya karibu na mipaka ya Ukraine, baada ya kumaliza luteka za kijeshi zilizoibua wasiwasi mkubwa kwa mataifa ya Magharibi

https://p.dw.com/p/47E2y
Russland | Truppenabzug | Panzer der russischen Armee werden auf Züge verladen
Picha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/picture alliance

Taarifa ya wizara ya ulinzi ya Urusi imesema mapema leo kwamba treni nyingine iliyobeba wanajeshi na vifaa vya vikosi vya vifaru vilivyokuwa vimepiga kambi eneo la magharibi imerejea kwenye kambi za kudumu zilizopo mkoa wa Nizhny Novgorod baada ya kukamilika kwa luteka hizo.

Soma pia: NATO yajitayarisha kupambana na kitisho cha Urusi Ukraine

Hata hivyo, imesema kwenye taarifa nyingine kwamba ndege za kivita zilikuwa zikiondolewa kutoka katika rasi iliyonyakuliwa na Urusi ya Crimea na kupelekwa kwenye viwanja vya ndege katika maeneo mengine, ikiwa ni sehemu ya luteka hizo za kijeshi.

Brüssel Nato-Treffen Verteidigungsminister
NATO inasema iko tayari kupambana na UrusiPicha: Olivier Matthys/AP/picture alliance

Hatua ya kuendelea kuwapunguza wanajeshi iliyotangazwa hii leo ni ya karibuni zaidi katika matangazo kadhaa kama hayo yaliyotolewa wiki hii, ambayo awali yaliibua matumaini ya kupunguza wasiwasi kati ya Urusi na Magharibi kuelekea Ukraine, ingawa Marekani ilisema Urusi haijafanya chochote kikubwa na badala yake inazidi kuongeza wanajeshi kwenye mipaka ya Ukraine.

Rais Vladimir Putin wa Urusi, anatarajiwa kusimamia luteka hizo hapo kesho, ambapo atashuhudia mazoezi ya urushwaji wa makombora yatakayofanywa na kikosi maalumu cha nyuklia, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la Urusi, Interfax.

Soma pia: NATO yahofia Urusi inatafuta kisingizio cha kuivamia Ukraine

Huku haya yakiarifiwa, huko Moscow, Rais wa Belarus Alexander Lukanshenko tayari amewasili mjini humo kwa mazungumzo na rais Putin kuhusiana na hatma ya wanajeshi wa Urusi walioko nchini humo, waliokuwa wakishiriki luteka hizo za kijeshi zilizopangwa kumalizika Jumapili hii.

Donbas | Pro-Russische Soldaten beobachten
Kumekuwa na mashambulizi mashariki UkrainePicha: Kisileva Svetlana/ABACA/picture alliance

Lukashenko alishawahi kusema wazi kuhusu uwezekano wa wanajeshi hao ambao ni sehemu ya wanajeshi wa Urusi waliopiga kambi kaskazini, kusini na mashariki mwa Ukraine kwamba wanaweza kubaki hapo kwa muda mrefu zaidi, na hapo jana alisema watajua hilo baada ya mazungumzo ya hii leo kati yake na Putin, ikiwa wataendelea kubaki kwa ama masaa, siku au hata miezi.

Amesema pia kwamba Moscow na Minsk wamekubaliana kuziacha silaha nchini Belarus na kwamba Minsk ama inaweza kuzinunua kutoka Urusi ama labda kuzichukua kama "zawadi".

Katika hatua nyingine, mawaziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu na wa Marekani Lloyd Austin wanatarajia kuzungumza kwa simu baadae leo, kufuatia ombi la Marekani, Interfax limeinukuu wizara ya ulinzi ya Urus, wakati mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa hayo Sergei Lavrov na Anthony Blinken pia wakipanga wiki ijayo kujadiliana tena kuhusu hali inavyoendelea katika mvutano huo wa Ukraine.

Lakini pamoja na wasiwasi ulioko huko nje, nchini Ukraine waziri wa ulinzi wa Oleksii Reznikov mapema leo ameliambia bunge la nchi hiyo kwamba taarifa za kiintelijensia za ndani zinaashiria kwamba kuna uwezekano mdogo wa kusambaa kwa mzozo kati yake na Urusi.

AFPE/RTRE/DPAE