1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yahofia Urusi inatafuta kisingizio cha kuivamia Ukraine

17 Februari 2022

Mawaziri wa ulinzi wa Jumuiya ya kujihami ya NATO wanakamilisha mkutano wao wa siku mbili mjini Brussels ambapo wameijadili hofu kuhusu uwezekano wa Urusi kutafuta kisingizio cha kuwatuma wanajeshi wake nchini Ukraine

https://p.dw.com/p/47BHp
Brüssel Nato-Treffen Verteidigungsminister
Picha: Olivier Matthys/AP/picture alliance

Washirika wa NATO wameituhumu Urusi kwa kuupotosha ulimwengu na Habari za uwongo kwa kusema kuwa inawaondoa baadhi ya wanajeshi wake na kuwarejesha makambini, wakihoji kuwa Moscow badala yake imeongeza karibu askari 7,000 zaidi karibu na mpaka wake na Ukraine unaoshuhudia mvutano.

Soma pia: NATO yajitayarisha kupambana na kitisho cha Urusi Ukraine

Huku hofu ya nchi za Magharibi ikiongezeka kuwa Urusi inapanga kuvamia, mivutano pia imeongezeka leo kwenye mstari unaowatenganisha wanajeshi wa Ukraine na wanaharakati wanaopigania kujitenga mashariki mwa nchi hiyo wanaoungwa mkono na Urusi, ambapo pande zote zimetuhumiana kwa mashambulizi makali.

Brüssel Nato-Treffen Verteidigungsminister
Washirika wa NATO wanapinga masharti ya UrusiPicha: Olivier Matthys/AP/picture alliance

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenbergamesema muungano huo wa kijeshi una wasiwasi kuwa Urusi inajaribu kuweka kisingizio cha kuanzisha shambulizi la kijeshi dhidi ya Ukraine

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amesema kumekuwa na Ushahidi wa wanajeshi wa Urusi kusogea karibu kabisa na mpaka wa Ukraine, kuwasili kwa wanajeshi Zaidi wakitumia ndege, wanaongeza hifadhi ya damu na hata kujiweka tayari katika Bahari Nyeusi. "Tumeona ripoti za mashambulizi ya makombora na zinasikitisha. Bado tunakusanya maelezo. Lakini unajua tumesema kwa muda sasa kuwa Warusi huenda wakafanya kitu cha aina hii ili kuhalalisha mzozo wa kijeshi. Kwa hiyo tutalifuatilia hilo kwa karibu sana."

Moscow imesema mara kadhaa wiki hii kuwa baadhi ya wanajeshi wake wanaondoka mpakani kurejea makambini, lakini haikutoa maelezo ambayo yangeweza kuthibitishwa kwa njia huru kuhusu idadi na mwelekeo wa uhamishwaji wa askari hao, na viongozi wa Magharibi mara moja wakaelezea mashaka yao kuhusu kauli hizo za Urusi.

Russland Truppenabzug Die Panzer der russischen Armee werden auf Bahnsteige verladen
Urusi inasema inawaondoa baasdhi ya askari wakePicha: AP/picture alliance

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kufanya baadae leo mkutano wa kila mwaka kuijadili hali ya mashariki mwa Ukraine.

Soma pia: NATO: Urusi yapeleka wanajeshi zaidi mpakani

Urusi inataka nchi za Magharibi kutoikaribisha katika NATO Ukraine na mataifa mengine yaliyokuwa sehemu ya muungano wa Kisovieti, kusitisha upelekaji wa zana karibu na mipaka ya Urusi na kuwaondoa wanajeshi kutoka mashariki mwa Ulaya, matakwa ambayo washirika wanayapinga vikali.

Makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa, kijeshi na kidiplomasia wanaoelekea leo kushiriki katika kongamano la kila mwaka la usalama mjini Munich ambalo litaujadili kwa kina mzozo huo wa Ukraine na Urusi.

ap, afp, dpa, reuters