1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroPakistan

Mzozo mpya waibuka kati ya Pakistan na Iran

18 Januari 2024

Mzozo mpya umeibuka kati ya Pakistan na Iran baada ya nchi hizo mbili kufanya mashambulizi ya kuvuka mpaka kwa kile wanachodai ni kukabiliana na makundi ya wanamgambo.

https://p.dw.com/p/4bPS4
Pakistan yafanya mashambulizi nchini Iran
Pakistan imefanya mashambulizi nchini Iran na kuwalenga wanamgambo wanaotaka kujitenga katika eneo la Sistan-Baluchistan 17.01.2024Picha: Tasnim

Pakistan imefanya mashambulizi nchini Iran hii leo, ikiwalenga wanaharakati wanaotaka kujitenga wanaofahamika kama Baloch. Hayo yameelezwa na Wizara ya mambo ya nje ya Pakistan, siku mbili tu baada ya Iran kushambulia ngome za kundi jingine la wanamgambo katika ardhi ya taifa la Pakistan na kusababisha vifo vya watoto wawili kwa mujibu wa serikali mjini Islamabad.

Vyombo vya habari vya Iran vimesema makombora kadhaa yalipiga kijiji kimoja

katika Jimbo la Sistan-Baluchestan ambalo linapakana na Pakistan, na kuua takriban watu tisa. Taarifa za awali zimesema wanawake watatu na watoto wanne waliuawa, na wote wakiwa si raia wa Iran.

Iran I Hussein Amirabdollahian akizungumza katika mkutano wa WEF huko Davos
Hussein Amirabdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, akizungumza katika Jukwaa la Kiuchumi la Dunia (WEF) mjini Davos, Uswisi.Picha: Hannes P Albert/dpa/picture alliance

Kwa upande wake, wizara ya mambo ya nje ya Pakistan imesema mashambulizi hayo yaliendeshwa kwa ufanisi na usahihi mkubwa na yalilenga maficho ya magaidi na kuwaua kadhaa. Jeshi la nchi hiyo limesema magaidi hao ni kutoka kundi linalojiita "Jeshi la Ukombozi wa Baluchistan".

Soma pia:Iran na Pakistan zatakiwa kujizuia kufuatia shambulio la anga

Wizara hiyo imeendelea kuwa inaheshimu uhuru na mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini ikasisitiza kuwa lengo pekee la kitendo cha leo lilikuwa kulinda usalama na maslahi ya Pakistan, ambayo imesema "ni muhimu na kamwe hayawezi kuathiriwa."

Mvutano wa kidiplomasia kati ya Pakistan na Iran

Pakistan I Wizara ya Mambo ya Nje mjini Islamabad
Askari Polisi akiwa nje ya jengo la Wizara ya mambo ya Nje ya Pakistan mjini Islamabad nchini Pakistan: 18.01.2024Picha: Anjum Naveed/AP/picture alliance

Pakistan ambayo inamiliki silaha za nyuklia, imemuita nyumbani mwanadiplomasia wake mkuu kutoka Tehran. Mumtaz Zahra Baloch, Msemaji wa Serikali ya Pakistan amesema:

"Tumewafahamisha pia kwamba Pakistan imeamua kumrejesha nyumbani Balozi wake kutoka Iran na kuhusu balozi wa Iran nchini Pakistan ambaye kwa sasa yuko ziarani huko Iran, ni vyema asirudi kwa muda huu."

Aidha, Waziri Mkuu wa muda wa Pakistan Anwaar-ul-haq Kakar amefupisha ziara yake nchini Uswisi ambako alikuwa akihudhuria Kongamano la Kiuchumi duniani huko Davos.

Soma pia: Iran yafanya mashambulizi dhidi ya wanamgambo Pakistan

Mahusiano kati ya majirani hao yamekuwa yakigubikwa mara kadhaa na mivutano, lakini mashambulizi ya hivi punde yanaarifiwa kuwa uvamizi wa hali ya juu zaidi katika miaka ya hivi karibuni.

Waziri Mkuu wa muda wa Pakistan Anwaar-ul-haq Kakar
Waziri Mkuu wa muda wa Pakistan Anwaar-ul-haq Kakar: Picha ya Agosti 12, 2023Picha: Senate of Pakistan/REUTERS

Mzozo huu kati ya Iran na Pakistan unazidisha wasiwasi wa kuchochea ukosefu wa utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati tangu kuibuka kwa mzozo wa Israel na kundi la Hamas. Inahofiwa pia mzozo huo kutanuka zaidi baada ya wanamgambo wenye mafungamano na Iran kutoka Lebanon, Syria, Iraq na Yemen kujitosa katika vita hivyo.

China ambayo ni jirani wa mataifa hayo na mshirika mkuu wa kibiashara imejitolea kuwa mpatanishi katika mzozo huu huku kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa mashambulizi zaidi ya kulipiza kisasi. China na Urusi ambazo zina ushawishi eneo hilo zimetoa wito wa kujizuia kwa pande zote mbili na kutoruhusu  kuongezeka kwa hali ya migogoro.

(Vyanzo: Mashirika)