1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar: Suu Kyi afungwa miaka 4 Jela

6 Desemba 2021

Mahakama ya kijeshi Myanmar, imemfunga kiongozi aliyeondolewa madarakani Aung San Suu Kyi miaka minne jela kwa makosa ya uchochezi na kupuuza masharti ya kupambana na virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/43ssd
Thailand Protest Myanmar Protest Aung San Suu Kyi
Picha: Sakchai Lalit/AP Photo/picture alliance

Rais wa Myanmar aliyeondolewa madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliofanyika Februari mosi Win Myint, pia amehukumiwa miaka minne jela hii ikiwa ni kulingana na mtu aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, wakati mahakama ilipokuwa inatoa hukumu yake ya kwanza, katika kesi kadhaa dhidi ya Suu Kyi na viongozi wengine wa kiraia waliokamatwa wakati wa mapinduzi.

Suu Kyi anakabiliwa na kesi kadhaa zinazojumisha mashitaka ya rushwa, ukiukaji wa sheria ya siri na mawasiliano pamoja na kupuuza masharti ya kupambana na virusi vya corona

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa wahofia uhalifu mkubwa kutendeka Myanmar

Wafuasi wake wamesema kesi hizo haina msingi wowote na zinalenga kummaliza kisiasa huku jeshi likiendelea kudhibiti madaraka. Naibu waziri aliye upande wa upinzani Maw Htun Aung, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba hakutarajia chochote kizuri kutoka kwa mfumo wa utawala mbovu Myanmar.

Amnesty International yasema huku dhidi ya Suu Kyi ni feki

Hongkong Schließung Büro Amnesty International
Nembo ya Amnesty International Picha: Vincent Yu/AP/picture alliance

Hata hivyo shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limesema hukumu dhidi ya Suu Kyi ni feki na kukielezea kifungo chake kama mfano wa hivi karibuni wa kusudio la jeshi kuuondoa upinzani na kukandamiza kabisa demokrasia.

Kulingana na Mkurugenzi wa kikanda wa shirika hilo Ming Yu Hah uamuzi huo ni sehemu ya mfululizo wa adhabu zinazotolewa Myanmar zilizosababisha watu 1,300 kuuwawa na maelfu kukamatwa tangu kutokea kwa mapinduzi. 

Naye Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binaadamu Myanmar Yanghee Lee amesisitiza hukumu iliyotolewa ni ya uonevu.

Hadi sasa jeshi la Myanmar halijatoa taarifa ya wapi alikozuiliwa Suu Kyi  huku wakili wake wakizuiliwa kuwasiliana na waandishi habari.

NLD haijatoa tamko kuhusu hukumu ya kiongozi wao

Mmoja ya waandamanaji akibeba picha ya Suu Kyi
Mmoja ya waandamanaji akibeba picha ya Suu KyiPicha: Jack Taylor/AFP/Getty Images

Myanmar imekuwa katika mgogoro tangu kulipofanyika mapinduzi dhidi ya serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Aung San Suu Kyi. Tangu wakati huo kumefanyika maandamano kote nchini humo ya kupinga mapinduzi hayo huku Jumuiya ya Kimataifa ikiingiwa na wasiwasi kuhusu kusitishwa kwa mabadiliko ya kisiasa kufuatia miongo kadhaa ya uongozi wa Kijeshi.

soma zaidi: Wamyanmar wakimbilia India kufuatia vurugu za jeshi

Kyi aliye na miaka 76 ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobeli amezuiliwa tangu Februari mosi pamoja na viongozi wengine wa juu wa chama chake cha NLD.

Viongozi wengine wamekimbilia mataifa ya nje na msemaji wa chama chake hakupatikana kutoa maoni kuhusu hukumu aliyopewa kiongozi wao.

Chanzo: afp/ reuters/ap