1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Umoja wa Mataifa wahofia uhalifu mkubwa kutendeka Myanmar

23 Oktoba 2021

Umoja wa Mataifa umesema unakhofia janga kubwa zaidi la haki za binaadamu nchini Myanmar, wakati kukiwa na taarifa za maelfu ya wanajeshi wanaolekea kaskazini mwa taifa hilo la kusini mashariki mwa Asia.

https://p.dw.com/p/425US
Russland 9. Moskauer Konferenz für internationale Sicherheit l Min Aung Hlaing, Myanmar
Picha: Sefa Karacan/Anadolu Agency/picture alliance

"Tunapaswa kuwa tayari kama watu wa eneo hili la Myanmar walivyojitayarisha, kwa uhalifu mkubwa wa halaiki. Ninatamani kwamba niwe siko sahihi," alisema Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Myanmar, Tom Andrews.

Zaidi ya raia 1,100 wameshauawa kwenye msako mkali dhidi ya wapinzani na wengine zaidi ya 8,000 wametiwa nguvuni tangu mapinduzi hayo, kwa mujibu wa kundi linalofuatilia hali ya mambo nchini Myanmar.

Andrews, ambaye alikuwa akiwasilisha taarifa ya kila mwaka juu ya haki za binaadamu ya Mnyanmar mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, alisema alikuwa amepokea taarifa kwamba makumi kwa maelfu ya wanajeshi wenye silaha nzito walikuwa wanaelekea maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa nchi yaliyo na upinzani mkali.

Mbinu kama za mauaji ya Warohingya

Screenshot UN-Sonderberichterstatter Tom Andrews
Tom Andrews, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Myanmar.Picha: UN Web TV

Uchunguzi uliofanywa, alisema, pia unaonesha kuwa utawala wa kijeshi wa Mnyamar ulikuwa unahusika na matendo ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu na uhalifu wa kivita.

"Mbinu hizi zinafanana sana na zile zilizotumiwa na jeshi kabla ya mashambulizi yake ya kimbari dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika Jimbo la Rakhine mwaka 2016 na 2017," alisema Andrews.

Kiasi cha Warohingya 740,000 walilikimbia jimbo hilo la Rakhine mwaka 2017 baada ya vikosi vya usalama kuanzisha msako mkali ambao Umoja wa Mataifa umesema ulikuwa sawa na mauaji ya kimbari.

Andrews aliyatolea wito mataifa wanachama kuunyima utawala wa kijeshi wa Myanmar fedha, silaha na uhalali inaoutaka, akitaja kitendo cha kuachiwa kwa baadhi ya wafungwa mapema wiki hii kama ushahidi wa jinsi shinikizo la kimataifa linavyofanya kazi.

Wafungwa 5,000 waachiliwa

Myanmar | Freilassung von Gefangenen
Baadhi ya wafungwa walioachiliwa huru na utawala wa kijeshi wa Myanmar.Picha: AFP/Getty Images

Siku ya Jumatatu (18 Oktoba), kiongozi wa kijeshi wa Myanmar, Min Aung Hlaing, alitangaza kuachiwa huru wa zaidi ya watu 5,000 waliokuwa wamefungwa jela kwa kuandamana dhidi ya mapinduzi yake ya kijeshi.

Uamuzi huo ulitangazwa siku chache kabla ya Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) kutangaza hatua ya kuutenga utawala huo wa kijeshi kabla ya mkutano wa kilele wa mataifa hayo kumi.

"Tangazo la ASEAN kwamba watawala wa kijeshi hawatakaribishwa kwenye mkutano ujao wa kilele lilipiga mahala ndipo," alisema Andrews.

Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa aliongeza kwamba vikosi vinavyodhibitiwa na jeshi vimewalazimisha watu robo milioni kuyakimbia makaazi yao. Wengi wa hao wamewaji kukamatwa, wakiwemo makumi ya waliopoteza maisha kutokana na mateso.

Andrews alisema amepokea taarifa za uhakika kuwa watoto pia wamekuwa wakiteswa na utawala wa kijeshi wa Myanmar.