1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshauri maalum ateuliwa kuchunguza kesi za Hunter Biden

12 Agosti 2023

Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Merrick Garland, amemteuwa mshauri maalum kwenye uchunguzi dhidi ya Hunter Biden, mtoto wa kiume wa Rais Joe Biden, katika hatua ya kushangaza kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2024.

https://p.dw.com/p/4V5Z4
Hunter Biden
Hunter BidenPicha: Jonathan Ernst/REUTERS

Katika taarifa yake iliyotolewa jana, Garland alisema kuna mazingira yasiyo ya kawaida kwenye suala hilo. Amemteuwa David Weiss ambaye tayari alikuwa anachunguza masuala ya kifedha ya Hunter Biden, baada ya makubaliano ya kukiri makosa kuvunjika. Mabadiliko haya ya matukio yamezusha maswali mapya kwenye kesi dhidi ya mtoto huyo wa rais wa sasa Marekani, zinazohusiana na ukwepaji kodi na kumiliki silaha, ambazo utatuzi wake ulikuwa karibu ufikiwe wiki chache zilizopita. Weiss mwenyewe, ambaye aliteuliwa kushika nafasi ya uwanasheria na rais wa wakati huo, Donald Trump, ndiye aliyeomba kuteuliwa kuwa mshauri maalum, kutokana na uzoefu mkubwa alionao kwenye uchunguzi dhidi ya Hunter Biden. Uchunguzi huu unakuja wakati Wizara ya Sheria ya Marekani ikiwa imechukuwa hatua zisizotarajiwa za kumshitaki Trump, hasimu mkubwa wa Biden kwenye uchaguzi uliopita na ujao, kwa kesi mbili za nyara za serikali na jaribio la kuzuwia matangazo ya uchaguzi.