1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwafrika wa Kwanza kuongoza ILO

Hawa Bihoga
25 Machi 2022

Waziri mkuu wa zamani wa Togo Gilbert Houngbo amechaguliwa kuongoza shirika la kazi duniani ILO, atakuwa mwafrika wa kwanza kuongoza shirika hilo kongwe la umoja wa mataifa.

https://p.dw.com/p/493ie
Gilbert Houngbo
Picha: DW/R. Guezodje

 

Mkuu huyo mpya ataanza kazi baadae mwaka huu baada ya mkuu wa sasa Guy Ryder raia wa Uingereza kumaliza muhula wake wa uongozi. 

Baada ya duru mbili za upigaji kura, bodi inayoongoza shirika hilo ilimchagua mzee huyo mwenye umri wa miaka 61 kumrithi mwanaharakati wa vyama vya wafanyakazi wa Uingereza Guy Ryder, ambae atatamatisha uongozi wake mwishoni mwa mwezi September baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka kumi kwenye ofisi hiyo.

Soma zaidi:Shirika la kazi duniani ILO laadhimisha miaka 100

Houngbo ambae kwa hivi sasa ni mkuu wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo wenye makao yake makuu mjini Roma (IFAD), alichaguliwa kutoka miongoni mwa wagombea watano na tangu awali alionekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo kutokana na kupata uungwaji mkono mkubwa na wafanyakazi pamoja na Umoja wa Afrika.

Mpambano katika mchakato wa uchaguzi

Wapinzani wake katika kinyang'anyiro hicho walikuwa waziri wa zamani wa kazi wa Ufaransa Muriel Penicaud, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Korea Kusini Kang Kyung-wha, mjasiriamali wa Afrika Kusini Mthunzi Mdwaba, na naibu wa ILO nchini Australia Greg Vines.

Schweiz | ILO verabschiedet ein neues Verfahren gegen Belästigung / Gewalt am Arbeitsplatz
Guy Ryder Mkurugenzi mkuu wa ILO akihutubia mkutanoPicha: Reuters/D. Balibouse

Ushindi wa Houngbo unaashiria mabadiliko makubwa kwa ILO, ambayo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1919 imekuwa ikiongozwa na wanaume kutoka Ulaya au Amerika pekee.

Soma zaidi:UN: Vifo 745,000 vimetokona na kufanya kazi sana

Shirika hilo kongwe zaidi la Umoja wa Mataifa lina nchi wanachama 187 na wajumbe 56 katika baraza la uongozi huku nusu yao wakiwakilisha serikali, na waliosalia wakiwakilisha waajiri na wafanyakazi.

Hotuba yake ya kwanza baada ya ushindi

Katika hotuba yake ya kwanza baada ya zoezi la upigaji kura na kuibuka na ushindi Houngbo alipongeza mchakato mzima wa uchaguzi. Alisema matokeo ya uchaguzi huo yana ishara nyingi ikiwemo kutimiza matarajio ya kijana wa kiafrika ambaye malezi yake ya unyenyekevu yaligeuka kuwa mafanikio ya haki kwa jamii.

Gilbert Fossoun Houngbo - Togos Ministerpräsident tritt zurück
Gilbert Fossoun Houngbo waziri mkuu wa zamani TogoPicha: AP

Awali mkuu wa sasa Guy Ryder akizungumza katika baraza lililoongoza uchaguzi huo alimsifu Houngbo kwa kuweka historia na aliona ni heshima kwa mkuu huyo mpya kuliongoza shirika hilo kongwe zaidi la umoja wa mataifa.

soma zaidi:ILO yalenga kuangamiza ajira ya watoto

Houngbo ambae atachukua usukani mnamo Oktoba mosi, atakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo marekebisho ya kanuni za shirika hilo zinazoshughulikia masuala ya ajira ulimwenguni katika kipindihichi ambacho mabadiliko ya teknolojiwa yanashuhuduwa kwa kasi.