1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano kati ya mfalme wa Jordan na kaka yake wasuluhishwa

6 Aprili 2021

Mazungumzo ya upatanishi kati ya mfalme Abdullah wa Jordan na kaka yake Mwanamfalme Hamza yamefanikiwa kutuliza mvutano uliojitokeza mwishoni mwa juma ambao ulitishia uthabiti wa kisiasa wa taifa hilo la kiarabu.

https://p.dw.com/p/3rbnz
Jordanien König Abdullah Prinz Hamzah al-Hussein 2012
Mfalme Abdullah wa Jordan (aliyevaa suti nyeusi) akiwa pamoja na wanafamilia wengine wakati wa harusi ya Mwanamfalme Hamza (aliyevalia kijeshi) mwaka 2012.Picha: Balkis Press/abaca/picture alliance

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Kasri la mfalme mjini Amman, mwafaka umepatikana baada Mwanamfalme Hamza kuahidi utiifu kwa mfalme Abdullah na kumaliza kile kilichotajwa kuwa moja ya mzozo mgumu zaidi wa kisiasa kwenye falme hiyo kiarabu ambayo ni mshirika muhimu wa mataifa ya magharibi kwenye kanda ya mashariki ya kati.

Taarifa hiyo imesema mwanamfalme Hamza ametia saini barua inayoahidi utii kwa mfalme wa nchi hiyo baada ya kufanyika mazungumzo kati yake na wanafamilia wengine wa falme ya Jordan.

Kwenye barua hiyo Hamza, ambaye ni kaka wa mfalme Abdullah na ambaye wakati fulani aliandaliwa kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo amesema yuko tayari kuheshimu katiba ya Jordan na kutii mamlaka ya kiongozi wake.

Mzozo huo ambao ni wa nadra ndani ya familia ya kifalme ya Jordan uliibuka Jumamosi iliyopita baada ya jeshi kumtuhumu mwanamfalme Hamza kupanga njama za kuteteresha uthabiti wa nchi hiyo na kuamuru kuwekwa kizuizini pamoja na kumpiga marufuku kujihusisha na shughuli zozote za kawaida.

Kupitia video alizorikodi kwa siri, Hamza alisema mkuu wa jeshi la Jordan alimwarifu kuwa haruhusiwi kutoka kwenye makaazi yake au kuwasiliana na watu wengine.

Tuhuma kuwa Mwanamfalme Hamza anafanya hujuma 

Jordanien Prinz Hamzah al-Hussein Royal Aero Sports Club 2012
Mwanamfalme Hamza wa Jordan Picha: Khalil Mazraawi/AFP

Mnamo siku ya Jumapili mamlaka za nchi hiyo zilisema zimegundua mpango wa kuvuruga utulivu wa taifa unamuhusisha mwanamfalme Hamza na kwamba uchunguzi uliofanyika umewezesha kukamatwa kwa watu kadhaa wenye nafasi nyeti kwenye utawala wa nchi hiyo. Madai hayo yalikanushwa mara moja na mwanamfalme huyo.

Licha ya matamshi makali aliyotumia Hamza kupitia mikanda yake ya video, mazungumzo ya upatanishi yameonesha kuzaa matunda na kumaliza mvutano wa hadharani baina ya mflame Abdullah na ndugu yake.

Mapema jana Mfalme Abdullah alimuomba mjomba wake mwanamfalme Hassan kusuluhisha mvutano uliojitokeza na katika kikao cha familia Hamza amesema yuko tayari kumuunga mkono na kumtii kaka yake ambaye ni mfalme wa nchi hiyo.

Kati ya mwaka 1999 hadi 2004 Hamza mwenye umri wa miaka 41 alikuwa kwenye nafasi ya kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Jordan kabla ya mfalme Abdullah kumuondoa kwenye orodha hiyo na kumtea mtoto wake wa kiume Mwanamfalme Al-Hussein.

Licha ya hatua hiyo, Hamza aliahidi kuwa mtiifu kwa mfalme Abdullah na amesalia kuwa mtu maarufu nchini Jordan na hata kwenye mvutano uliojitokeza amepata uungwaji mkono mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kwa kukemea vitendo vya rushwa nchini humo.

Migawanyiko kwenye taifa muhimu kwenye kanda ya Mashariki ya Kati 

Jordanien Proteste
Picha: picture-alliance/dpa

Mzozo wa mwishoni mwa juma umedhihirisha migawanyiko iliyomo kwenye taifa hilo linalozingatiwa kuwa kitovu cha uthabiti kwenye kanda ya mashariki ya kati.

Kwenye mvutano huo Marekani, mataifa ya eneo la Guhuba, Misri na Umoja wa nchi za kiarabu kwa pamoja ziliahidi kumuunga mkono mfalme Abdullah. Ujumbe kama huo uliotolewa pia na Urusi jana Jumatatu.

Jordan ina idadi ya watu milioni 10 lakini ina nafasi muhimu katika kanda ya mashariki ya kati inayoandamwa kila mara na mizozo.

Inapakana na Israel, ukingo wa magharibi, Syria, Iraq na Saudi Arabia na ni mwenyeji wa vikosi vya jeshi la Marekani na inawahifadhi mamilioni ya wapalestina waliotafuta hifadhi ya kisiasa pamoja na wakimbizi kutoka Syria.

Mwandishi :Rashid Chilumba/AFP/DPA/Reuters

Mhariri: