1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jordan yarejesha udhibiti wa maeneo yanayolimwa na Israel

Yusra Buwayhid
12 Novemba 2019

Wakulima wa Israel wamepata pigo kubwa Jumapili, Mfalme wa Jordan alipotangaza kumalizika kwa miaka 25 ya makubaliano yaliyowaruhusu kulima katika maeneo mawili ya Jordan ya al-Ghamr and al-Baqura yaliyo mpakani.

https://p.dw.com/p/3Sonp
Israel Jordanien Brücke über den Fluß Jordan mit Flaggen
Picha: AP

Chini ya mpango huo, sehemu ya makubaliano ya amani ya mwaka 1994 kati ya Israel na Jordan, maeneo hayo mawili ya mpakani yanatambuliwa kuwa chini ya utawala wa Jordan, lakini wakulima wa Israel wamepewa ruhusa maalumu ya kulima ardhi hiyo.

Hata hivyo, mnamo mwaka 2018, Jordan ilikataa kuyarefusha makubaliano hayo. Hatua iliyoangaliwa kama ishara ya kuongezeka kwa mvutano wa kidiplomasia kati yao.

Katika hotuba yake ya kufungua kikao cha kwanza cha bunge, Mfalme Abdullah jana alitangaza rasmi mwisho wa makubaliano hayo ya miaka 25.

"Ninatangaza mwisho wa kunyakuliwa maeneo haya mawili, Ghumar na Al-Baqoura, katika makubaliano ya amani na sasa Jordan itachukua udhibiti kamili kwa kila inchi ya maeneo hayo," amesema Mfamle huyo.

"Uamuzi huo ni pigo kubwa kwetu," anasema Eli Arazi ni mkulima mwenye umri wa miaka 74. Arazi analima katika eneo la Baqoura linalojulikana kwa Kiyahudi kama Naharayim lenye maana ya mito miwili. Kwa vile eneo hilo linapatikana kati ya Mto Yarmouk na Mto Jordan.

Palästina Israel | Konflikte | Nethanjahu genehmigt vor Wahl israelische Siedlung von Mevoot Jericho im Westjordanland
Bonde la Jordan ambalo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametishia kulinyakuaPicha: Getty Images/AFP/J. Ashtiyeh

Mkulima huyo anasema kwa miaka 70 wamekuwa wakipanda mazao kama vile mizaituni, ndizi pamoja na maparachichi.

Mahusiano ya kidiplomasia sio mazuri

Waisraeli wanadai haki ya umiliki binafsi wa eneo hilo tangu miaka ya 1920, wakati eneo hilo lilipokuwa sehemu ya Palestina chini ya utawala wa Uingereza.

Jordan ni mojawapo ya nchi mbili pekee za Kiarabui zenye makubaliano ya amani na Israel. Lakini raia wake wengi hawafurahishwi na makubaliano hayo kutokana na wengi wao kuwaunga mkono watu wa Palestina.

Hata hivyo, Jordan imesema itaendelea kuheshimu haki za umiliki wa ardhi za Waisraeli katika eneo hilo. Lakini kuanzia sasa watalazimika kukaguliwa mpakani kama wageni wengine.

Licha ya Isarel kuomba kurefushiwa mkataba huo, Jordan ilikataa ombi hilo. Mahusiano kati yao kwa sasa sio mazuri. Jordan imekasirishwa na matamshi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika kampeni zake za uchaguzi uliopita wa Septemba alipoahidi kulikamata kwa nguvu bonde la Jordan.

Vyanzo: dpa, rtre