1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUjerumani

Kansela Scholz aonya dhidi ya kuupuuza uwezo wa Afrika

20 Novemba 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameonya dhidi ya kudharau uwezo wa watu wa Afrika, wakati akiwakaribisha viongozi wa Kiafrika mjini Berlin kwa mkutano wa kilele wa Ushirikiano kati ya nchi za G20 na bara la Afrika.

https://p.dw.com/p/4ZE4J
Deutschland Bundeskanzler Olaf Scholz (SPD)
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Akizungumza kwenye jopo la majadiliano katika kongamano hilo la uwekezaji, Scholz amewashauri viongozi wa kibiashara walio na nia ya kuwekeza barani Afrika kuwa hali ya baadae ya Afrika inaonyesha matumaini. Lakini alisisitiza kuwa utawala wa sheria ni nguzo muhimu kwa makampuni ya Ujerumani. "Jumuiya ya wafanyabiashara iliyokusanyika hapa inaelewa haswa kwamba kipengele muhimu zaidi kwa mazingira mazuri ya biashara ni utawala wa sheria, kwamba unaweza kutegemea kile mulichokubaliana. Na kupata maendeleo katika nyanja hizi na kufanya mageuzi mwafaka ya kiuchumi pia ni muhimu.

Soma pia: Mkutano wa uwekezaji Afrika wafanyika Berlin

Kauli hizo za Scholz zimejiri baada ya kuahidi dola bilioni 4.4 kwa ajili ya miradi ya mazingira kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya ifikapo mwaka wa 2030. Ili kuwa wazi kabisa, hii haihusu misaada ya maendeleo kulingana na mpango wa kizamani wa wafadhili na wapokeaji. Hii ni kuhusu uwekezaji unaolipa pande zote mbili."

Kansela huyo wa Ujerumani ameongeza kuwa viongozi wanapaswa kuonyesha jinsi ukuaji, maendeleo ya kijamii na kiuchumi vinaweza kufanya kazi kwa Pamoja bila kuharibu mazingira.

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier
Rais Steinmeier ausifia ushirikiano wa Afrika na UlayaPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Naye Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameunga mkono ushirikiano wa karibu kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika. Steinmeier amesema pande zote zina uzito kwenye jukwaa la dunia kama zitaweka wazi na kutekeleza misimamo yao ya Pamoja.

Steinmeier amesema "Mkataba na Afrika" kimsingi unahusu kuimarisha uhusiano wa kiuchumi. Amesema kwa sasa asilimia 40 ya uwekezaji unaofanywa barani Afrika tayari unatoka Umoja wa Ulaya. Bara la Afrika lina uwezo mkubwa, hasa linapokuja suala la nishati mbadala. Hii inatumika, kwa mfano, kwa maeneo ya nishati ya jua na upepo, kwa matumizi ya nishati ya joto na kwa malighafi ambayo hutumiwa katika paneli za jua au betri. Umoja wa Ulaya umezifanya nchi za Kiafrika kuwa mshirika halisi katika mabadiliko ya sekta ya nishati duniani.

Soma pia: EU kuekeza zaidi ya dola milioni 60 kwa umeme Uganda

Mkutano huo unahusu Mkataba huo wa Ushirikiano na Afrika, ambao ulizinduliwa kwenye mkutano wa kundi la nchi 20 zilizostawi kiviwanda la G20 mjini Hamburg miaka sita iliyopita. Mataifa 13 ya Kiafrika sasa yanashiriki.

Katika hotuba yake, Rais Steinmeier aliyazungumzia masharti ya kutoka upande wa Afrika ya kuondokana na migawanyiko ya kawaida ya majukumu kati ya wafadhili na wapokoeaji ambayo imezoeleka katika miongo ya karibuni. Ili kufanikisha hilo, amesema Ujerumani lazima ielewe ukweli na kushughulikia historia yake ya enzi ya ukoloni, ambayo ilikuwa na sifa ya machafuko na ukandamizaji dhidi ya Waafrika. Anaongeza kuwa bila kuashughulikia yaliyopita huko nyuma, hakuna ushirikiano wa kweli utakaowezekana.

Wakati huo huo, Rais huyo wa shirikisho la Ujerumani aliwakimbusha washiriki kuwa nchi za Kiafrika zinachangia asilimia nne pekee ya uzalishaji wa gesi ya kaboni duniani, lakini wakati huo huo huathirika hasa kutokana na matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi na matukio mabaya ya hali ya hewa.

Steinmeier ametoa mifano ya maafa ya mafuriko yaliyotokea kwenye pwani ya Afrika Kaskazini na pia ukame mbaya zaidi wa hivi karibuni kuwahi kutokea katika kanda ya Afrika Mashariki katika miaka 40

afp, dpa, ap, reuters