1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya kwanza ya ubakaji wa ndani ya ndoa Eswatini

Yusra Buwayhid
17 Januari 2020

Ufalme wa Eswatini unaimarisha haki za wanawake walioolewa. Taifa hilo limeanzisha sheria ya kuwafungulia mashtaka waume wanaowabaka wake zao -- hatua iliyowakasirisha wengi kwenye jamii ya Swati ya kihafidhina.

https://p.dw.com/p/3WN9e
Swasiland | König Mswati III
Picha: Getty Images/AFP/G. Guerica

Wiki hii, mwanamume wa miaka 34 Nhlanhla Dlamini alikuwa mtu wa kwanza kushtakiwa kwa madai ya ubakaji kwa kufanya tendo la ndoa na mkewe bila ya idhini yake.

Kwa kutumia Sheria ya Makosa ya Kijinsia na Vurugu za Nyumbani (SODV) ya mwaka 2018, ambayo inakataza tendo la ndoa kati ya mume na mke bila ya kupatikana idhini, polisi walimtia mbaroni Dlamini na kumshitaki kwa kosa la ubakaji.

Siku ya Jumanne (14 Januari), Mahakama Kuu ya mji mkuu wa Mbabane ilimuachilia kwa dhamana ya dola za Kimarekani 3,400, na alitakiwa kurudi mahakamani wiki chache baadaye.

"Ni kesi ya kwanza kurekodiwa na kusikilizwa mbele ya mahakama ya wazi," msemaji wa Kikundi cha Swaziland cha Hatua Dhidi ya Dhuluma (SWAGAA) Slindelo Nkosi aliliambia shirika la habari la AFP.

Watenda uhalifu wa mara ya kwanza wanaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 20 jela, wakati wahalifu waliorudia kosa hilo wanaweza kufungwa hadi miaka 30.

Kesi hiyo ya kihistoria ilishangaza wengi kote nchini humo. Taifa hilo pekee la kifalme barani Afrika, lililokuwa likijulikana kama Swaziland, linatajwa kuwa na utamaduni uliozoeleka wa mfumo dume.

Kiongozi wake, Mfalme Mswati III, ameoa wake 14 tangu alipovishwa taji la ufalme mnamo mwaka 1986 akiwa na umri wa miaka 18. Ana watoto wanaozidi 25. Anatajwa kupenda maisha ya strarehe, huku asilimia 63 ya raia milioni 1.3 wa nchi yake wakiwa wanaishi katika hali ya umaskini.

"Sheria hii ni kinyume na maadili ya utamaduni wetu wa asili kama Waswazi," alisema mfanyabiashara Sabelo Mahlangu akizungumza na shirika la habari la AFP.

"Huwezi kuniambia kwamba mke niliyemuoa kwa kumlipia mahari, kulingana na mil mila na desturi zetu, anaweza kusema mume wake amembaka."

"Upuuzi gani huo?" anauliza. "Hata Biblia inaonya dhidi ya wanandoa kunyimana haki yao ya tendo la ndoa."

Mitazamo hiyo ya Mahlangu inaungwa mkono kote nchini humo.

Swasiland | Großmutter mit Kind nahe der Hauptstadt Mbabane
Mwanamke akiwa na mtoto karibu na mji mkuu wa MbabanePicha: picture-alliance/Photoshot/B. Coleman

Wanawake waifurahia

Katika mtandao wa kijamii wa Facebook, Ndosi Shenge, aliwasisitiza wanaume kuwa na wanawake kadhaa "ili mmoja anapokuwa hataki kufanya tendo la ndoa, mwanamme aweze kwenda kwa mpenzi wake mwengine".

Lakini kwa mjane na mama wa watoto wawili, Sizakele Langa, sheria ya SODV ni muhimu katika kuwalinda wanawake walio kwenye ndoa "kwavile kwa miaka mingi wanaume wamekuwa wakiwanyanyasa wanawake bila ya kuwajibishwa kwa namna yoyote ile".

Langa alisema alikuwa ametoka kwenye ndoa ya miaka 12, baada ya kuchoka kubakwa na mume wake.

"Alikuwa na kawaida ya kutaka kufanya tendo la ndoa kwa lazima kila baada ya ugomvi kati yetu.. Ninapomkatalia hunikamata kwa nguvu," aliliambia shirika la habari la AFP, na kuongeza kwamba alikuwa akizidiwa nguvu, naye hakutaka kupiga kelele kwa kuhofia kuwaamsha watoto wake wanaokuwa wamelala.

"Familia yangu isingeniamini kwamba mume wangu akinibaka, hata polisi pia wasingeniamini."

Unyanyasaji wa kijinsia ni kitu cha kawaida katika taifa hilo lilozungukwa na mataifa mengine ikiwa ni pamoja Msumbiji pamoja na Afrika Kusini. Lakini ni nadra kwa wahalifu wa tendo hilo kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kulingana na takwimu za polisi za mwaka 2019, katika kipindi cha miezi saba Eswatini ilirikodi visa 2,900 vinavyoangukia kwenye sheria hiyo ya SODV.

Mkurugenzi wa kikundi cha watafiti cha Wanawake na Sheria nchini Afrika Kusini, Colane Hlatshwayo, alisema ni inashtusha kuona kwamba jamii inaliangalia kosa la ubakaji wa wanawake kama kitu cha kawaida kwa sababu tu wanawake hao wamo ndani ya ndoa.

Changamoto ni kwamba "mmoja wao ana nguvu zaidi ndani ya ndoa na anaamini hahitaji idhini ya mwenziwe kufanya tendo la ndoa," alisema Hlatshwayo.

Nkosi wa kikundi cha SWAGAA alilieleza tatizo hilo la ubakaji wa ndani ya ndoa kuwa linasababisha mabishano makubwa kwavile watu wengi bado hawajalielewa vizuri.

"Kuna hisia mbaya ya umiliki inayoongezeka miongoni asilimia fulani ya wanaume, haswa baada ya kuhalalisha uhusiano wake na mwanamke baada ya kuilipa familia yake mahari.

"Mtazamo huu umechangia kuongezeka kwa manyanyaso ndani ya ndoa kwa sababu mmoja wao anaamini anamliki mwenziwe," amesema Nkosi.

Chanzo: AFP