1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msumbiji: Raia sita wauawa kwa kukatwa vichwa

Zainab Aziz Mhariri: Daniel Gakuba
8 Septemba 2022

Watu sita wameuawa kikatili baada ya waasi wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS) kuuvamia mji mmoja katika jimbo la Nampula nchini Msumbiji. Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amesema mashambulizi hayo ni ya kigaidi.

https://p.dw.com/p/4Gb3I
Mosambik Rede Präsident Filipe Nuysi
Picha: Sitoi Lutxeque/DW

Akizungumza katika mji wa mapumziko wa Xai Xai kaskazini mwa mji mkuu Maputo, Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amesema waasi hao walifanya mauaji hayo wakati wakiwakimbia wanajeshi wa Msumbiji, Rwanda na wale wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambao wanajumuisha kikosi cha kupambana na vurugu katika eneo la kaskazini mwa Msumbiji ambako uasi umekithiri katika jimbo la Cabo Delgado. Tangu vurugu zilipoanza mnamo mwaka 2017 maelfu ya watu wamepoteza maisha na miradi ya gesi asilia ya thamani ya mabilioni ya dola imesambaratika.

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amesema kuanzia siku ya Jumamosi iliyopita jimbo la Cabo Delgado limekabiliwa na mashambulizi mapya ambayo ameyataka kuwa ni mashambulizi ya kigaidi  Raia wengine watatu walitekwa nyara lakini pia magaidi sita wamekamatwa. Katika wilaya mbili za Erati na Memba katika jimbo la Nampula nyumba kadhaa zilichomwa moto.

Baadhi ya raia wa jimbo la Nampula waliogeuka kuwa wakimbizi wa ndani nchini Msumbiji.
Baadhi ya raia wa jimbo la Nampula waliogeuka kuwa wakimbizi wa ndani nchini Msumbiji.Picha: Roberto Paquete/DW

Wakati huo huo ripoti za vyombo vya Habari vya nchini Msumbiji, zilizothibitishwa na Waziri wa mambo ya nje wa jimbo la Nampula, Mety Gondola, zinasema mtawa mmoja raia wa Italia aliyekuwa na umri wa miaka 83, aliuawa kwa kupigwa risasi. Mtawa huyo aliishi katika mji wa Nacala, na aliuawa katika shambulio la siku ya Jumanne usiku ambapo wamishonari wawili walifanikiwa kukimbia.

Shirika la Habari la Ureno -Lusa, limesema mtawa huyo, aliyeuawa kwa kupigwa risasi kichwani alikuwa anatumikia Misionari ya Comboni Sisters na amekuwa akifanya kazi nchini Msumbiji tangu mwaka 1963.

Soma:Tanzania kuchangia kupambana na ugaidi nchini Msumbiji

Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS limethibitisha kuhusika na mauaji ya mtawa huyo na Wakristo wengine watatu wakati wapiganaji wake walipouvamia mji wa Nacala katika jimbo la Nampula siku ya Jumanne. Kundi hilo pia limedai kuwa wapiganaji wake walilichoma kanisa, hospitali, majengo mengine kadhaa, magari mawili pamoja na mali nyingine za kanisa katika mji huo.

Eneo la Kaskazini mwa Msumbiji limekumbwa na mfululizo wa mashambulizi yanayohusiana na watu wenye itikadi kali za kidini tangu mwaka 2017. Lakini eneo la Nampula ambako hadi sasa lilikuwa limeepuka ghasia mbaya ambazo sana zinalikumba jimbo jirani la Cabo Delgado lenye utajiri wa gesi.

Mpho Molomo, Mkuu wa ujumbe unaopambana na vurugu nchini Msumbiji (SAMIM) wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Mpho Molomo, Mkuu wa ujumbe unaopambana na vurugu nchini Msumbiji (SAMIM) wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).Picha: DW

Umoja wa Ulaya umesema utatoa msaada wa ziada kwa muungano wa kijeshi wa Afrika huko nchini Msumbiji, wakati ambapo mashambulizi ya kundi la IS yakionekana kutishia miradi gesi inayoyokusudiwa kuzipunguzia nchi za Umoja wa Ulaya kutegemea nishati kutoka Urusi.

Mnamo mwezi uliopita wa Agosti, serikali za Umoja wa Ulaya zilithibitisha kukubali kutoa euro milioni 15 kuusaidia ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa Msumbiji (SAMIM), ambayo inapambana na waasi wenye itikadi kali kaskazini mwa Msumbiji.

Vyanzo:RTRE/AFP