1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLithuania

Mshirika wa Navalny ashambuliwa nchini Lithuania

13 Machi 2024

Mpinzani mashuhuri wa Urusi Leonid Volkov, mshirika wa marehemu Alexei Navalny, amevunjwa mkono baada ya kushambuliwa nje ya nyumba yake katika mji mkuu wa Lithuania.

https://p.dw.com/p/4dTUW
Leonid Volkov, mshirika wa marehemu Alexei Navalny
Leonid Volkov, mshirika wa marehemu Alexei Navalny akizungumza na wanahabari mjini Vilnius, Lithuania.Picha: Gerhard Mey/REUTERS

Kamishna wa Polisi  wa Lithuania Renatas Pozela amesema wanatumia "rasilimali nyingi" kuchunguza shambulio lililofanyika mjini Vilnius dhidi ya Leonid Volkov, msaidizi wa muda mrefu wa aliyekuwa kiongozi wa upinzani wa Urusi marehemu Alexei Navalny.

Katika ujumbe wa video kwa njia ya mtandao wa Telegram, Volkov alisema alipigwa mara 15 kwenye mguu wakati wa shambulio hilo, na mkono wake ukavunjwa siku ya Jumanne.

Tukio hilo limeibua taharuki kutoka kwa serikali ya Lithuania. Idara ya ujasusi ya Lithuania inasema kuna uwezekano mkubwa Urusi ndiyo iliyohusika na shambulio hilo.

Soma pia: Navalny azikwa mjini Moscow

Baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini siku ya Jumatano, Volkov alisema, "tutafanya kazi na hatutakata tamaa," akielezea shambulio hilo kama "salamu za majambazi " kutoka kwa wafuasi wa Putin.

Mke wa Volkov, Anna Biryukova, awali alichapisha picha za majeraha ya mumewe kwenye mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na jicho jeusi, alama nyekundu kwenye paji la uso na mguu uliovuja damu na iliyolowa hadi kwenye suruale yake.

Kabla ya tukio hilo msemaji wa Navalny Kira Yarmysh pia aliripoti kwamba "mtu fulani alivunja dirisha la gari na kumpulizia kitoa machozi " kabla ya kumpiga kwa nyundo.

Mshukiwa wa tukio hilo bado hajatambuliwa.

Idara za kijasusi nchini humo zilisema shambulio dhidi ya mwanaharakati anayeishi Lithuania "huenda" ilikuwa operesheni "iliyoandaliwa na kutekelezwa na Urusi, ambayo madhumuni yake yalikuwa kusimamisha utekelezaji wa miradi ya upinzani dhidi ya Urusi."

Washirika wa Navalny wameishutumu Urusi kwa kumuua kiongozi wa upinzani mwenye umri wa miaka 47, ambaye alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 19 jela kwa mashtaka ya itikadi kali kabla ya kifo chake  mwezi Februari katika jela ya adhabu kali.

Leonid Volkov ni nani?

Leonid Volkov, katika Bunge la Ulaya huko Strasbourg Disemba 15,2021.
Mpinzani mashuhuri wa Urusi Leonid Volkov, mshirika wa marehemu Alexei Navalny. Picha: Jean-Francois Badias/AP/picture alliance

Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 43 ni miongoni mwa viongozi mashuhuri wa upinzani nchini Urusi na alikuwa mtu wa karibu wa Navalny. Alikuwa mmoja wa wakuu wa zamani wa kiongozi huyo na mwenyekiti wa Wakfu wa Kupambana na Ufisadi hadi 2023.

Volkov aliondoka Urusi mnamo 2019 chini ya shinikizo kutoka kwa mamlaka.

Mnamo 2021, Urusi iliamuru waranti ya kukamatwa kwa Volkov katika maeneo yote ya Jumuiya ya Madola Huru (CIS). Wakimtuhumu "kuwachochea watoto kuandamana."

Mwaka jana, yeye na timu yake walizindua mradi unaoitwa "Navalny's Campaigning Machine," kwa lengo la kuwashawishi raia wengi iwezekanavyo wa Urusi , ama kwa simu au mtandaoni, kumpinga Putin kabla ya uchaguzi wa rais.

Mara kwa mara Volkov aliwahi kukabiliwa na mashtaka ya jinai na mamlaka ya Urusi , ikiwa ni pamoja na kifungo cha siku 20 jela ambacho kilimzuia kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa Deutsche Welle wa Global Media Forum.

https://p.dw.com/p/4dSR5