Mpinzani wa Putin Navalny ahamishiwa gereza Aktiki
25 Desemba 2023Mamlaka zilimhamisha mwanasiasa mashuhuri wa upinzani nchini Urusi hadi gereza lililojitenga katika eneo la aktiki, miezi mitatu kabla ya kura ya urais inayotarajiwa kumpa Vladimir Putin muhula wa tano kwa urahisi.
"Tumempata Alexei Navalny," mshirika wake, Kira Yarmysh, alisema kwenye mtandao wa kijamii.
"Hivi sasa yuko IK-3 katika makazi ya Kharp katika Wilaya huru ya Yamalo-Nenets," Yarmysh aliongeza. "Wakili wake alimtembelea leo. Alexei anaendelea vizuri."
Wilaya ya Kharp, ambayo ni nyumbani kwa takribani watu 5,000, iko juu ya Mzingo wa Aktiki.
Soma pia:Navalny amkejeli Putin, ''Mfalme yuko uchi''
Ni "mojawapo ya makoloni ya kaskazini na ya mbali," alisema Ivan Zhdanov, ambaye anasimamia Wakfu wa Kupambana na Ufisadi wa Navalny.
"Mazingira ya huko ni magumu sana, na utawala maalum katika eneo la baridi kali" na mawasiliano kidogo sana na ulimwengu wa nje, alisema Zhdanov.
Navalny alihamasisha maandamano makubwa dhidi ya serikali kabla ya kufungwa jela mwaka 2021, baada ya kunusurika katika jaribio la kumuua kwa sumu.
Alianza kutumia muda mwingi wa kuzuiliwa kwake katika koloni la adhabu la IK-6, takriban kilomita 250, mashariki mwa Moscow katika mkoa wa Vladimir. Mahakama ilirefusha kifungo chake kwa miaka 19 kwa makosa ya itikadi kali.
Pia iliamua kwamba ahamishwe kwenye gereza kali zaidi la utawala maalum, ambalo kwa kawaida huwekwa wafungwa hatari.
Baada ya wiki kadhaa za kutokuwa na uhakika, Navalny alipatikana katika gereza la IK-3, maarufu kama "Polar Wolf" - ambalo ni koloni kali la utawala.
Anaweza kuhamishiwa koloni la karibu la Nambari.18 -- "Polar Owl" -- ambalo lina utawala mkali hata zaidi.
Ukosefu wa taarifa wazusha wasiwasi
Ni jambo la kawaida kwa uhamishaji kuchukua wiki kadhaa nchini Urusi, kwa sababu wanafungwa wanasafirishwa taratibu kwa njia ya reli kati ya magereza yalioko maeneo ya mbali.
Lakini ukosefu mkubwa wa taarifa juu ya aliko kumeibua wasiwasi kutoka kwa washirika wake, makundi ya haki na serikali za mataifa ya Magharibi.
Marekani ilisema Jumamosi "ilikuwa na wasiwasi mkubwa" kuhusu hali hiyo. Washirika wake walisema walikuwa wametuma maombi kwa zaidi ya vituo 600 vya magereza.
"Kulikuwa na marufuku kamili ya taarifa kumhusu," Zhdanov alisema. Washirika wanaamini Kremlin ililenga kumtenga zaidi mkosoaji huyo wa sauti.
"Tangu mwanzo, ilikuwa wazi kwamba viongozi walitaka kumtenga Alexei, hasa kabla ya uchaguzi," Zhdanov pia alisema. Urusi itapiga kura ya urais Machi 2024, inayotarajiwa kumpa Putin muhula wa tano kwa urahisi.
Vyama kadhaa washirika wa Kremlin vinatarajiwa kusimamisha wagombea kwa ajili ya kura ya Machi, lakini upinzani wa kweli umetengwa.
Soma pia: Mahakama ya EU yalaani shambulizi la sumu la Urusi la 2020
Moscow kwa miaka mingi imedhoofisha wanasiasa na wanaharakati huru wa Urusi, hali ambayo iliongezeka baada ya Kremlin kuamuru wanajeshi wa Urusi kuivamia Ukraine mnamo 2022. Vuguvugu la Navalny limelengwa hasa kwa ukandamizaji wa Kremlin.
Hata kabla ya uvamizi nchini Ukraine, shirika la Navalny lilitangazwa kuwa la msimamo mkali, hali ambayo iliwezesha kufunguliwa mashtaka kwa wanachama na wafuasi wake.
Wakuu kadhaa wa mikoa wa Wakfu huo wa Kupambana na Rushwa walifungwa jela.
Miongoni mwao ni Lilia Chanysheva, mshirika wa Navalny katika Jamhuri ya Bashkortostan ya kati, ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka saba na nusu gerezani msimu huu wa joto.
Washirika wengi mashuhuri wamekimbia, akiwemo Maria Pevchikh, ambaye anaendesha Wakfu wa Kupambana na Rushwa kutokea nje ya nchi na alilengwa na kibali cha kukamatwa cha Urusi wiki iliyopita.
chanzo: AFPE