1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Umoja wa mataifa jua ya mkataba unaopiga marufuku utapakazaji silaha za kinuklea.

Mohammed Abdulrahman2 Mei 2005

Tangu kusainiwa 1970 mkataba huo amekua ukilega- lega , kama si kushindwa kabisa kufanya kazi.

https://p.dw.com/p/CHgy
mmoja wa waandamanaji, wapinzani wa silaha za kinuklea nje ya makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini Newyork.
mmoja wa waandamanaji, wapinzani wa silaha za kinuklea nje ya makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini Newyork.Picha: AP

Nchi zipatazo 190 zinaanza mkutano hii leo mjini New York, utakaotathimini mkataba unaopiga marufuku utapakazaji wa silaha za kinuklea, huku mgogoro mkubwa zaidi ukiwa kati ya Marekani na Korea kaskazini pamoja na Iran. Hali hiyo inadhihirisha jinsi juhudi za kuzuwia utapakazaji wa silaha za Atomiki zinavyokabiliwa na matatizo makubwa.

Tangu uliposainiwa, Ulimwengu umekua ukikabiliwa na enzi mpya ya kile kinachoitwa na Marekani “Mataifa maovu,“ magenge ya kimataifa ya biashara ya magendo ya silaha za aina hiyo, na makundi ya kigaidi ya kimataifa yanayotafuta silaha za kinuklea.

Shirika moja la kupigania amani lenye makao yake makuu mjini Washington-Marekani , limesema“ Dunia imebadilika, lakini utawala hazijabadilika na kwenda sambamba na mabadiliko hayo duniani.“ Matukio katika siku chache za nyuma linasema shirika hilo yameonyesha wazi jinsi hali ilivyo mbaya .

Kabla ya mkutano huo kwenye makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini Newyork, Marekani iliripoti kwamba kombora moja la masafa mafupi lilifyatuliwa jana kutokea pwani ya mashariki ya Korea kaskazini. Lilikwenda umbali wa kilomita 100 na kuangukia katika eneo la bahari a Japan.

Wakati mnadhimu mkuu katika Ikulu ya Marekani Andrew Card akitamka hayo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha CNN, msemaji wa Wizara ya mambo ya nchi za nje ya

Marekani Kurtis Coope naye, alisema wamekua na wasi wasi kwa muda mrefu na mpango wa kinuklea wa Korea kaskazini pamoja na harakati zake kwa jumla, na akaitaka nchi hiyo isitishe majaribio yake ya makombora yenye uwezo wa kutoka eneo moja hadi jengine.

Korea Kaskazini iliushituwa Ulimwengu Agosti 1988, kwa kufyatua kombora la masafa marefu katika anga ya Japan, ambalo liliangukia katika bahari ya Pacific.

Kwa wakati huu taifa hilo halikaguliwi kimataifa kuhusu harakati zake za Kinuklea, baada ya kujitoa kutoka Shirika la kimataifa la nguvu za atomiki Desemba 2002 na kujiondoa katika mkataba wa kimataifa unaopiga marufuku utabakazaji wa silaha za kinuklea mwezi uliofuata. Korea kaskazini sasa inadai kwamba ina silaha za Atomiki.

Iran nayo kwa upande mwengine iko katika hali ya mvutano panapohusika mkataba huo unaopiga marufuku usambazaji wa silaha za kinuklea, huku Marekani ikidai kwamba nchi hiyo ya Ghuba inatengeneza kwa siri za atomiki, chini ya kisingizio cha kwamba mpango wake una malengo ya amani , ukiwa na madhumuni ya kuongeza kiwango chake cha nishati. Kwa maneno mengine ni mpango wa kiraia unaoweza kukaguliwana Shirika la kimataifa la nguvu za atomiki.

Umoja wa Ulaya ukiungwa mkono na Marekani unaitaka Iran kuzuwia harakati zote za kurutubisha mafuta yanayotumiwa kwa madhumuni ya kinuklea. Badala yake Umoja wa ulaya kupitia mazungumzo yalioanza Desemba mwaka jana na Iran, iko tayari kuipa nchi hiyo msaada wa kiuchumi, usalama na teknolojia.

Iran imesema hatua yake ya wakati huu kuzitisha shughuli za kuyarutubisha maadini ya Uranium ni ya muda na ya hiyari- Wakati ikisisitiza kwamba ni haki yake chini ya msingi ya Shirika la kimataifa la nguvu za Atomiki kuendesha shughuli za kinuklea kwa malengo ya amani.

Mkataba unaopiga marufuku utapakazaji wa silaha za kinuklea, ulipata pigo kubwa miaka miwili iliopita, ulipogunduliwa mtandao wa soko la magendo la kimataifa la teknolojia inayoweza kutumiwa kutengeneza silaha za atomiki, akihusika muasisi wa bomu la atomiki Pakistan Abdul Qadeer Khan ambaye anasemekana alizipatia ufundi huo, Korea Kaskazini, Iran na Libya.

Wataalamu pamoja na hayo wana shaka shaka kama mkutano huo wa mwezi mmoja kuutathimini mkataba huo unaopiga marufuku utapakazaji wa silaha za kinuklea kweli utaweza kuleta marekebisho yanayohitajika.Huo ni mkutano wa saba wa aina yake tangu 1970-ukifanyika kila baada ya miaka mitano.

Jana maelfu ya waandamanaji walikusanyika karibu na makao makuu ya umoja wa mataifa mjini Newyork, wakidai kukon´golewa kwa silaha zote za kinuklea, kote duniani.