1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Mazingira COP 27 waelekea ukingoni

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
14 Novemba 2022

Mkutano kuhusu hali ya hewa waeleka ukingoni nchini Misri. Matarajio ni madogo juu ya suala la malipo ya fidia kutokana na uharibifu uliosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi maskini.

https://p.dw.com/p/4JTun
COP27 - Weltklimagipfel 2022
Picha: MOHAMMED SALEM/REUTERS

Wajumbe katika mkutano huo unaoendelea hadi siku ya Ijumaa kwenye mji wa mapumziko wa Sharm el-Sheikh nchini Misri, kwa mara ya kwanza wamekubali kuliweka suala hilo la ufadhili kutokana na hasara na uharibifu kwenye ajenda ya mkutano huo. Nchi zinazoendelea zimekuwa zikishinikiza kwa muda mrefu kuundwa mfumo wa kifedha utakaozingatia utaratibu wa kushughulikia madhara yanayotokana na hali ya hewa katika nchi maskini.

Hata hivyo, kundi la kimataifa linalotetea mazingira, Greenpeace, limezilaumu nchi kadhaa tajiri, zikiwemo Marekani na Uingereza kwa kufubaza kimakusudi hatua za maendeleo ya kuanzishwa kituo cha hasara na uharibifu katika mkutano huo wa COP27. Greenpeace imeserma nchi hizo zinatumia mbinu za kuchelewesha mambo mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa makubaliano juu ya suala hilo hayafikiwi na hivyo yaahirishwe labda mpaka angalau mwaka 2024.

Mwanaharakati wa mazingira kutoka Uganda Leah Namugerwa kwenye Mkutano wa COP27 nchini Misri.
Mwanaharakati wa mazingira kutoka Uganda Leah Namugerwa kwenye Mkutano wa COP27 nchini Misri.Picha: Sean Gallup/Getty Images

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, aliwatahadharisha viongozi wa dunia mapema kwamba kupata matokeo halisi juu ya suala hilo utakuwa ni mtihani mkubwa kwa serikali za mataifa yaliyojitolea kwa ajili ya mafanikio ya COP27.

Luc Gnacadja, Katibu Mtendaji wa zamani, kuhusiana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa amesema bara la Afrika linawakilisha asilimia 17 ya watu wote duniani, lakini linachangia asilimia tatu tu ya uzalishaji wa gesi chafu Gnacadja amesema kwa wakati huu, kutokana na kile kinachotokea duniani kote kuhusu athari za hali ya hewa na ongezeko la joto ni lazima sote tuungane kuzifanikisha hatua za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa na kwamba sote tufanye tuwezalo kulisaidia bara la Afrika kufuata njia sahihi za kujilinda ili kuepuka uzalishaji wa hewa ya kaboni.

Soma Zaidi: COP27: Kiwango cha uzalishaji gesi chafu kiko juu kabisa

Wanaharakati wa kutetea ulinzi wa mazingira wameongeza shinikizo kwa wajumbe katika mkutano huo kuyashurutisha mataifa kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, ikiwa ni pamoja na kusitisha ufadhili wa nishati za mafuta na gesi.

Vijana watetezi wa mazingira wanasisitiza hoja zao katika mkutano wa Misri wa COP27
Vijana watetezi wa mazingira wanasisitiza hoja zao katika mkutano wa Misri wa COP27Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, umesababisha kupanda kwa bei ya nishati ulimwenguni hali inayoyafanya mataifa kadhaa kufikiria upya juu ya sera zao za nishati na baadhi ya nchi ulimwenguni zimeamua kuiwasha upya mitambo yao ya nishati ya makaa ya mawe. Mkutano wa COP27 unafanyika huku dunia ikikumbwa na majanga ya asili yakiwemo mafuriko, joto kali na ukame, ambayo yanaathiri sana maisha ya watu kote ulimwenguni.

Vyanzo: DPA/RTRE