1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa nchi za Amerika ya kusini na Umoja wa ulaya mjini Guadalajara

28 Mei 2004

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na wenzao wa Latin America na visiwa vya Caribian wanakutana Guadalajara nchini Mexico kuzungumzia,biashara ya pande mbili,nafasi ya jumuia ya kimataifa na juhudi za kupambana na uonevu na dhuluma.

https://p.dw.com/p/CEI1
Pascal Lamy
Pascal LamyPicha: AP

Hii ni mara ya tatu kwa mkutano kama huu kuitishwa tangu ulipoanzishwa mwaka 1999,lakini ni mara ya kwanza kati ya viongozi 33 wa nchi za Latin America na visiwa vya Caribian na umoja wa Ulaya wenye wanachama 25-maeneo mawili yenye jumla ya wakaazi bilioni moja.

Licha ya kutokuwepo mkutanoni rais Fidel Castro wa Cuba, waziri mkuu wa Uengereza Tony Blair na kiongozi wa serikali ya Italy Silvio Berlsconi,mkutano huo wa kilele umegeuka kua fursa kwa kiongozi mpya wa serikali ya Hispania Jose Luis Rodriguez Zapatero kujitokeza kwa mara ya kwanza katika jukwaa la kimataifa.

Mjini Guadalajara,mji wa pili muhimu wa Mexico,mashuhuri kwa wambaji wa nyimbo za kiasili Mariachis na kinywaji cha Tekila,waziri mkuu wa seerikali ya Hispania atapata fursa ya kuonana pia na rais Jacques Chirac wa Ufaransa,kansela Gerhard Schröder wa Ujerumani na rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil.

Mada tatu muhimu katika mkutano huu wa viongozi ni kuhusu biashara huru,kuhifadhiwa usemi wa walio wengi ulimwenguni huku bendera ikishikiliwa na umoja wa mataifa kwa kutilia maanani kwamba umoja wa Ulaya,nchini za Latin America na Caribian zinawakilisha kwa pamoja thuluthi moja ya viti ndani ya umoja wa mataifa,na hatimae mshikamano wa jamii.

Vita vya Iraq na utovu waliofanyiwa wafungwa katika jela nchini humo ni miongoni mwa mada zinazojadiliwa pia .Azimio la Guadalajara litakalotangazwa baadae hii leo linatazamiwa kulaani visa hivyo japo kama Marekani haitatajwa kwa jina.

"Wanaobidi kulaaniwa ni waasisi wana majina, na sio wananchi wa nchi fulani au taifa fulani " amesema hayo kiongozi wa serikali ya Hispania Jose Luiz Zapatero.

Katika kikao cha maandalizi hapo jana mawaziri wa nchi za Latin Amerika ,visiwa vya Caribian na Umoja wa ulaya wameonyesha ishara ya kutaka kufikia makubaliano ya kutia njiani mfumo wa soko huru kati yao hadi ifikapo mwezi october mwaka huu .

Kamishna wa ulaya anaeshughulikia masuala ya biashara Pascal Lamy,amesema mwishoni mwa mazungumzo yao, azma ya kutia njiani mfumo wa soko huru kati ya nchi za Umoja wa ulaya na Latin Amerika utatajwa taarifa ya mwisho itakapotangazwa baadae hii leo.

Hata hivyo bwana Pascal Lamy amekiri kuna mengi yanayobidi kukamilishwa kabla ya makubaliano kufikiwa .Duru za kuaminika zinasema duru nyengine ya mazungumzo kati ya nchi za Amerika ya kusini na umoja wa ulaya itafanyika mjini Buenos Aires kuanzia wiki ijayo.Mazungumzo ya kutia njiani mfumo wa soko huru kati ya kambi hizi mbili yameanza tangu miaka minne iliyopita.

Itafaa kusema hapa kwamba mkutano wa kwanza wa viongozi wa nchi za umoja wa ulaya,Latin America na visiwa vya Caribian ulifanyika mwaka 1999 mjini Rio de Janeiro na kufuatiwa miaka mitatu baadae mjini Madrid.

Wakati huo huo watu sabaa wamejeruhiwa kidogo kufuatia machafuko kati ya makundi ya vijana wa chuo kikuu cha Mexico na vikosi vya polisi vilivyojaribu kuwatawanya wasaipige kambi karibu na mahala mkutano wa viongozi unakofanyika.

Hakuna aliyekamatwa.Mashirika kadhaa yasiyomilikiwa na serikali yanapanga kuitisha mikutano baidi sambamba na mkutano wa kilele wa Guadalajara.