1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa dharura wazungumzia mzozo wa kiutu Gaza

Sylvia Mwehozi
11 Juni 2024

Viongozi wanaohudhuria mkutano wa dharura wa kilele kuhusu mzozo wa kiutu wa Gaza nchini Jordan, wameahidi hii leo kutoa msaada mkubwa katika eneo hilo lililokumbwa na vita,

https://p.dw.com/p/4gvUU
UNRWA, Rafah
Wapalestina wakijaribu kufikia msaada wa chakula RafahPicha: Abed Rahim Khatib/Anadolu/picture alliance

Jordan imewaalika viongozi mbalimbali wa ulimwengu kushiriki mazungumzo ya dharura wakati mashirika ya misaada yakionya kwamba hali inazidi kuwa mbaya zaidi huko Gaza kuliko ilivyowahi kushuhudiwa, huku idadi ya wakaazi zaidi ya milioni mbili wakitegemea misaada ya hapa na pale. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza hadhara ya mkutano huo kwamba kasi na ukubwa wa mauaji huko Gaza vinashtua na "hofu lazima ikomeshwe." Katibu huyo mkuu ameunga mkono mpango wa usitishaji mapigano wa rais Biden, ambao Israel itapaswa kuondoa vikosi vyake kutoka Gaza na Hamas kuwaachia huru mateka kwa mabadilishano ya wafungwa.

Mahmud Abbas |Pedro Sanchez
Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas alipokutana na waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez huko JordanPicha: Thaer Ghanaim/AFP

Hata hivyo afisa mmoja katika serikali ya Israel aliyezungumza na shirika la habari la DPA, amesema kuwa mpango huo uliopendekezwa na Rais wa Marekani Joe Biden haupishani na malengo ya Israel katika vita hivyo. "Israel haitokomesha vita kabla ya kutimiza malengo yake ya vita, kuteketeza uwezo wa kijeshi na uongozi wa Hamas, kuwakomboa mateka wote na kuhakikisha Gaza haitoi tena kitisho kwa Israel katika siku zijazo."Blinken: Mataifa ya Kiarabu yaishinikize Hamas kukubali mpango wa upatanishi

Naye mratibu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths, amevielezea vita vya Gaza kama "doa dhidi ya ubinadamu" na kutoa wito wa kukusanywa kiasi cha Dola bilioni 2.5 kuweza kufikia mahitaji ya kiutu kwa watu wa Gaza kutoka mwezi Aprili hadi Desemba. Mfalme Abdullah II wa Jordan na rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi, wote pia wameunga mkono miito ya usitishaji mapigano. Rais Sisi hata hivyo ameionyeshea kidole Israel kuwa ndio imechochea mzozo huo wa kiutu na kuishutumu kwa kutumia njaa kama silaha ya vita.

"Ni muhimu kwa Israel kukomesha hali ya mzingiro na kuacha kutumia njaa kama silaha ya kuwaadhibu watu wa Ukanda wa Gaza, na kuilazimisha kuondoa vikwazo vyote, endelevu na vya kutosha vya misaada ya kibinadamu huko Gaza kutoka vivuko vyote na masharti muhimu kwa ajili ya usambazaji wa msaada kwenye ukanda huu wa Gaza na mikoa yake yote."

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

Katika mkutano huo, waziri wa masuala ya kigeni wa Marekani Antony Blinken alitangaza ahadi ya dola milioni 404 katika msaada mpya kwa watu wa Palestina, na kuzitaka nchi nyingine zikiwemo wakosoaji wa Washington kuchangia fedha kushughulikia mzozo wa kibinadamu wa Gaza. Msaada huo, unafanya jumla ya mchango wa Marekani kwa Wapalestina, huko Gaza, Ukingo wa Magharibi na kanda hiyo kufikia dola milioni 674 tangu vita vilipozuka mwezi Oktoba.

Soma pia: Hamas yaitaka Marekani kuishinikiza Israel kusitisha vita Gaza

Wakati huo huo, wizara ya afya huko Gaza inayoendeshwa na Hamas imesema kwamba watu wasiopungua 37,164 wameuawa katika miezi minane ya vita kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas.