1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kutoa motisha kwa ajili ya uwekezaji Afrika

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
9 Desemba 2022

Uwezekano wa Ujerumani kuwekeza barani Afrika umepigiwa debe kwenye mkutano wa kilele wa siku mbili baina pande hizo mbili uliofanyika mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/4KjLp
Südafrika Johannesburg | Bundeswirtschaftsminister Robert Habeck in Südafrika
Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Mkutano huo wa kilele kati ya Ujerumani na bara la Afrika unaofanyika kila baada ya miaka miwili huwaleta pamoja viongozi wa serikali na wafanyabiashara wa Afrika na Ujerumani. Kwa upande wa Ujerumani mkutano huo ni tukio kubwa kabisa la kibiashara barani Afrika. Waziri wa uchumi wa Ujerumani Robert Habeck alipoufungua mkutano huo wa kilele wa siku mbili alitoa kauli chanya na miito ya matumaini.

Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Robert Habeck
Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Robert HabeckPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Waziri Habeck amesema serikali ya Ujerumani imejiandaa kutoa motisha zaidi kwa ajili ya vitega uchumi kwenye maeneo kama ya Kusini mwa Afrika ambapo inakusudia kuhimiza uwekezaji wa Ujerumani. Amesema muhimu zaidi ni kuzingatia sera nzuri na thabiti katika mfumo wa uwekezaji.

Waziri Habeck pia ameongeza kusema kwamba kampuni za Ujerumani ziliwekeza dola bilioni 1.6 kwenye nchi za Afrika. Hata hivyo ameeleza kuwa kiwango hicho bado hakijatosheleza. Waziri wa uchumi wa Ujerumani Robert Habeck ametoa wito wa mwanzo na mtazamo mpya katika uhusiano kati ya Ujerumani, bara Ulaya na bara la Afrika.

Waziri huyo ametoa kandarasi ya kwanza ya kuagiza nishati ya Hydrogeni ya thamani ya Euro milioni 900. Kwa upande wake waziri wa biashara wa Afrika Kusini, Ebrahim Patel amesisitiza kuwa panahitajika ushirikiano zaidi na nchi nyingine ili kuleta maendeleo na neema. Waziri huyo wa Afrika kusini amesema pana fursa ya kuongeza biashara baina ya Ujerumani na nchi za Afrika. Ameeleza kuwa hatua imepigwa katika kuendeleza mauzo ya bidhaa kutoka Afrika kwenda Ujerumani.

Kushoto: Waziri wa uchumi wa Ujerumani Robert Habeck. Kulia: Waziri wa biashara wa Afrika Kusini, Ebrahim Patel.
Kushoto: Waziri wa uchumi wa Ujerumani Robert Habeck. Kulia: Waziri wa biashara wa Afrika Kusini, Ebrahim Patel. Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Hata hivyo ameshauri kwamba hatua ndefu zaidi zinapaswa kuchukuliwa. Amesema kuhusu vitega uchumi vya Ujerumani duniani kote kwa jumla, fungu la Afrika asilimia moja tu. Amesema pamoja na kuwa kidogo, kiwango hicho kimebakia pale pale kwa muda wa miaka mingi.

Nusu ya vitega uchumi kutoka Ujerumani vinaelekezwa nchini Afrika Kusini ambako kampuni zaidi ya 400 za Ujerumani zinatoa ajira kwa watu wapatao 65,000. Waziri Robert Habeck ambaye pia ni makamu wa Kansela wa Ujerumani, pia amesisitiza juu ya kuwekwa mfumo imara wa sheria, kuheshimiwa haki za binadamu, kuupiga vita ufisadi na kutenda haki kwa kampuni za ndani na za kutoka nje.