1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa China alihutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa

28 Septemba 2018

Wawakilishi wa China na Urusi leo Ijumaa wanatarajiwa kulihutubia baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Nchi hizo mbili zinawakilishwa na mawaziri wake wa mambo ya nje. Wang Yi wa China na Sergei Lavrov wa Urusi.

https://p.dw.com/p/35fcm
USA China - Chinesischer Außenminister Wang Yi
Picha: Getty Images/L. Zhang

Muda mfupi kabla ya kuingia studioni, Waziri wa mambo ya nje wa China ndiye aliyekuwa jukwaani, akilihutubia baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Katika hotuba yake,waziri huyo, Wang Yi amelenga kupinga ujumbe uliofikishwa na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye alishikilia sera yake ya Marekani kwanza, akizilaumu nchi nyingine kwa kuweka mbele maslahi yao.

Wang amesema ulimwengu wa leo umejaa nguvu za kuyumbisha utengamano, na kutoa wito wa jumuiya ya kimataifa kushikamana badala ya kila nchi kujichukulia mambo kivyake. Waziri huyo wa China amesema China itaendelea kuheshimu sheria na kanuni za kimataifa, na kukemea wale wanaozishurutisha nchi nyingine kufuata matakwa yao.

Awali, Waziri Wang Yi alikanusha madai kwamba nchi yake inaiba teknologia za kampuni za Marekani, mzozo ambao umesababisha Marekani kuiwekea China vikwazo. Waziri Wang amesisitiza kwamba China haijanakili hati miliki za nchi za nje na wala haitafanya hivyo na amesema haitataka nchi nyingine inakili hati miliki za China. Waziri Wang aliyasema hayo mbele ya baraza la mahusiano ya nje mjini New York ambako anahuhduria vikao vya baraza kuu la Umoja wa Mataifa.Urusi inatarajia kuzingatia katika hotuba yake kwa viongozi wa ulimwengu kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kwamba ina ushawishi mkubwa wa kama wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati hadi Venezuela na mpaka katika Rasi ya Korea.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei LavrovPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Zemlianichenko

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov amefanya mikutano ya pande mbili pembezoni mwa mkutano huo mkuu katika Baraza kuu la Umoja wa Mataifa wiki hii. Lavrov pia alitetea mikakati ya Urusi katika mikutano kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Wajumbe wengine watakao lihutubuia Baraza kuu la Umoja wa mataifa jioni hii ni pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas anayemwakilisha kansela Angela Merkel.

Rais Donald Trump wiki hii aliituhumu China kwamba inajiingiza katika uchaguzi wa Marekani utakaofanyika katikati ya mwaka, huku akisema ana ushahidi, lakini mpaka sasa bado hajautoa.

Wakati huo huo tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imepiga kura na kuamua kuendeleza uchunguzi wa kimataifa wa uhalifu dhidi ya binadamu unaotendekaka nchini Yemen licha ya upinzani mkubwa kutoka Saudi Arabia na washirika wake.

Nchi 21 zilipiga kura kuunga mkono hoja ya kuendelea na uchunguzi nchi 8 zilipinga, na nchi 18 hazikushiriki, kwa sababu zinapendelea kuwepo azimio jipya juu ya uchunguzi utakaosimamiwa na Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mwandishi:Zainab Aziz/AP/AFPE

Mhariri: Gakuba, Daniel