1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misururu ya mashambulizi yaendelea kushuhudiwa nchini Pakistan.

29 Mei 2009

Wanamgambo nchini Pakistan wameapa kuendelea na mashambulizi hayo ili kulipiza kisasi harakati za kijeshi zilizoendeshwa na serikali ya Pakistan katika bonde la Swat.

https://p.dw.com/p/Hzx9
Moto wawaka katika eneo kulikotokea shambulozi la bomu katika mji wa Peshawar.Picha: AP

Idadi ya watu waliouawa kutokana na misururu ya mashambulizi kaskazini mashariki mwa Pakiastan imefikia watu kuni na tano. Watu zaidi ya mia moja walijeruhiwa kwenye mashambulizi hayo yaliyofanyika katika miji ya Peshawar na Dera Ismail Khan.

Mashambulizi haya yamezusha hofu ya hatua za wanamgambo za kulipiza kisasi oparesheni iliyofanywa na vikosi vya serikali dhidi ya wapigani wa Taliban katika bonde la Swat.

Ghasia zinazoendeshwa na wanamgambo nchini Pakistan, taifa lililo na nguvu za kinyuklia na mshirika mkubwa wa Marekani, zilianza mwaka 2007 wakati mashambulizi yaliendeshwa dhidi ya jeshi la Pakistan, maeneo ya serikali pamoja na vituo vinavyomilikiwa na nchi za magharibi.

Pakistan ni muhimu kwa Marekani katika juhudi zake za kupambana na kundi la al-Qaeda na pia katika mipango yake za kusitisha harakati za kundi la Taliban nchini Afghanistan.

Kumeshuhudiwa takriban mashambulizi manane yaliyoendeshwa na wanamgambo tangu jeshi la Pakistan lianzishe vita katika bonde la Swat mwezi uliopita.

Muda mfupi baada ya bomu kuripuka katika mji wa Peshawar, mshambuliaji mwingine wa kujitolea mhanga alijiripua katika eneo tofauti la mji huo na kuwaua wanajeshi watatu .

Mashambulizi hayo yalitekelezwa saa chache baada ya kundi la Taliban kutangaza kuwa lilihusika na shambulizi lingine la kujitolea mhanga katika mji wa Lahore sîku ya jumatano, ambapo watu 24 waliuawa, likisema kuwa lilikuwa lilinalipiza kisasi harakati za jeshi la Pakistan katika bonde la Swat.

Mjini Peshawar, mabomu yaliyokuwa yamefungwa kwenye pikipiki yaliwaua watu sita na kuwajeruhi wengine sabini na pia kusababisha uharibifu mkubwa.

Anschläge in Pakistan
Mtu alijeruhiwa na shambulizi la bomu akipelekwa hospitalini.Picha: AP

Baadaye wanamgambo waliokuwa wamejihami wakiwa juu ya mapaa ya majumba, walianza kuwafyatulia risasi polisi waliokuwa chini. Picha za vituo vya runinga zilionyesha polisi wakijibu mashambulizi hayo.

Kulinagana na taarifa za polisi ni kuwa muda mfupi baada kituo cha polisi kushambuliwa, bomu lingine liliripuka katika mji ulio kaskazini magharibi wa Dera Ismail na kuwaua watu wanne na kuwajeruhi wengine sita.

Siku ya Jumatano jeshi la Pakistan lilitoa kile ambacho lilitaja kuwa ni ujumbe wa mawasiliano ya simu kati ya msemaji wa Taliban katika bonde la Swat, Muslim Khan, na mwanamgambo ambaye hakufahamika, ambapo Khan alisema kuwa wanajeshi watashambuliwa.

Mashambulizi yatafanywa nyumbani kwa wanajeshi ili watoto wao wauawe, ndio wafahamu…Khan alisema kwenye ujumbe huo uliopeperushwa na vyombo vya habari.

Wakati huo huo, serikali ya Pakistan imetangaza zawadi ya dola 60,000 kwa yeyote atakayetoa habari za kukamatwa kwa kiongozi wa kundi la Taliban katika bonde la Swat, Fazlullah, na washirika wake karibu 20.

Jeshi la Pakistan linasema kuwa wanamgambo 1,100 wameuawa pamoja na wanajeshi 60 katika mapigano hayo ya bonde la Swat, huku zaidi ya watu milioni 2.4 wakiyakimbia makwao.

Mkuu wa Uratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, John Holmes, alisema kuwa kuna jumla ya kambi 26 zinazowahifadhi watu 220,000 na kuongeza kuwa umoja wa mataifa umekusanya asilimia 21 ya dola milioni 543 unazohitajhi ili kuwahudumia walioathirika na mapigano hayo.

Mwandishi: Jason Nyakundi/RTR

Mhariri: Mohamed AbdulRahman