1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miito ya ufadhili ili kudhibiti ongezeko la joto la dunia

Saleh Mwanamilongo
3 Oktoba 2022

Nchi zinazoendelea zimetoa mwito wa kuwepo na ongezeko la ufadhili ili kupunguza joto duniani na kupambana na athari zake. Mwito huo umetolewa leo mjini Kinshasa.

https://p.dw.com/p/4Hh9W
BG Gasometer Oberhausen
Picha: Martin Meissner/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Mazingira wa Kongo Eve Bazaiba alitoa wito kwa nchi tajiri kuheshimu ahadi za kifedha na kuidhinisha mipango ya kusaidia kufidia uchafuzi wa hali ya hewa. Aliongeza kuwa fedha za kulinda misitu ya mvua inayonyonya kaboni ambayo Kongo ina maeneo makubwa inapaswa kuonekana si kama msaada lakini kama uwekezaji katika mustakabali wa binadamu.

''Tunahitaji kutumia maliasili zetu na kutafuta mkate kwa watoto wetu, lakini katika kutekeleza jukumu hili kuna vikwazo zaidi na zaidi vinavyohusishwa na hitaji la kupunguza uzalishaji wetu wa gesu chafu.  Nchi kadhaa za Kiafrika zinajitahidi kufanya chaguo kati ya kuishi kwa wakazi wao na udhibiti wa uzalishaji wa gesi chafu, wakati bara linawajibika kwa 4% tu ya uzalishaji wa gesi chafu duniani.  Nini cha kufanya katika hali hii? Kunyonya rasilimali zetu na kuwalisha watoto wetu au kuwatazama na kuwaua kwa njaa ?"

Ahadi ambayo haijatekelezwa

Niederlande Africa Adaptation Summit in Rotterdam
Picha: ANP/IMAGO

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry, pia alisisitiza haja ya fedha zaidi, akibainisha ahadi ambayo haijatekelezwa iliyoanzia kwenye mkutano wa COP15 huko Copenhagen mwaka 2009, ya kuzipa nchi zinazoendelea dola bilioni 100 kwa mwaka kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kwa upande wake, naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed alitoa picha mbaya kuhusu vita dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni. Akisema viashiria vyote vya hali ya hewa viko kwenye mwelekeo mbaya.

Wajumbe kutoka zaidi ya nchi 50 wanahudhuria mazungumzo hayo yasiyo rasmi ya siku mbili mjini Kinshasa, akiwemo mjumbe wa hali ya hewa wa Marekani John Kerry. Tukio hilo litakamilika Jumatano kwa majadiliano ya kando.