1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miili ya raia 50 yagunduliwa katika makaburi Kongo

Sylvia Mwehozi
19 Januari 2023

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wamegundua miili ya karibu raia 50 kwenye makaburi ya watu wengi huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya mkururo wa mashambulizi yanayofanywa na waasi.

https://p.dw.com/p/4MPqM
DR Kongo | Unruhen in Nord-Kivu
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Miili hiyo imegunduliwa na askari wa kulinda amani wakati walipokuwa wakifanya doria katika jimbo lililokumbwa na machafuko la Ituri kufuatia mashambulizi yanayoshukiwa kufanywa na kundi la wanamgambo la CODECO. Kulingana na naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq, makaburi hayo ya watu wengi yaliyokuwa na miili ya raia 42 wakiwemo wanawake 12 na watoto sita yamegunduliwa katika kijiji cha Nyamamba. Kaburi jingine lililokuwa na miili ya wanaume saba liligunduliwa kwenye kijiji cha Mbogi.

Farhan Haq amenukuliwa zaidi akisema kwamba, "matukio haya yalitokea katikati mwa hali ngumu ya kudhoofika kwa usalama katika maeneo ya Djugu na Mahagi. Tangu Desemba mwaka 2022, ujumbe wa kulinda amani umeripoti angalau raia 195 kuuawa, 68 kujeruhiwa pamoja watu 84 kutekwa wakati wa matukio kadhaa yanayohusishwa na makundi yenye silaha ya CODECO na Zaire. Mashambulizi ya hivi karibuni yameongeza idadi ya watu waliokosa makaazi kufikia milioni moja na nusu Ituri na kupunguza upatikanaji wa usaidizi wa kiutu kwa walio na uhitaji."

Afisa huyo ametaka kufanyike uchunguzi utakaoelezea ikiwa kuna uhusiano kati ya makaburi hayo na mashambulizi. Ameongeza kuwa "Monusco inaunga mkono mfumo wa mahakama wa Congo kuchunguza mashambulizi na kutaka wahusika kuwajibishwa".

DR Kongo weitere Tote nach einem Massaker bei Ituri
Raia na wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu wakihudhuria mazishi ya watu 62 waliouawa 2022 mjini IturiPicha: Jorkim Jotham Pituwa/AFP via Getty Images

Ituri, jimbo lililokumbwa na machafuko linalopakana na Uganda, limeshuhudia mkururo wa ghasia katika wiki za hivi karibuni, baada ya mauaji ya mwalimu wa jamii ya kabila la Lendu kuchochea mashambulizi ya kulipa kisasi kutoka kwa wanamgambo wa CODECO, linalodai kuwakilisha kabila hilo. Makabila ya Lendu na Hema kwa muda mrefu yamekuwa na uhasama ambao umesababisha maelfu ya vifo kati ya mwaka 1999 hadi 2003 kabla ya uingiliaji kati wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Ulaya.

Machafuko yalirejea tena mwaka 2017 yakihusishwa na kuzuka upya kwa kundi la CODECO. Kundi jingine la wanamgambo la Zaire nalo linasema kwamba linawakilisha jamii ya watu wa Hema. Mwanaharakati wa masuala ya haki za binadamu jimboni Ituri Dieudonne Lossa, amesema zaidi ya raia 80 wameuawa tangu mapema mwezi Januari.

Mamlaka za ndani zimeongeza kwamba wanamgambo wa CODECO pia waliwateka idadi kubwa ya wanawake wakati walipovishambulia vijiji. Mwezi Juni mwaka jana, vikundi saba vilivyogawika kutoka CODECO vilitangaza kukomeshwa kwa machafuko dhidi ya raia huko Iturihaswa katika eneo la Djugu ambako walikuwa wakiendesha operesheni zao. Lakini hata hivyo kundi hilo linaonekana kurejesha taratibu mashambulizi katika eneo hilo.