1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaazi wa Ituri walalamikia ukosefu wa Usalama wa eneo hilo

16 Februari 2022

Wakaazi wa Ituri katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, wamelalamikia kukosekana kwa usalama wa kudumu mkoani humo kaskazini-mashariki mwa nchi. Mkoa ambao bado uko chini ya utawala wa kijeshi kwa zaidi ya miezi tisa.

https://p.dw.com/p/477ML
UN-Mission in Kongo unter Druck - Milizen geben Waffen ab
Picha: epa Gare/dpa/picture-alliance

Wakazi wa Ituri wamechoshwa na mauaji ya mara kwa mara yanayoendeshwa kila siku na makundi yenye kumiliki silaha, yakiwemo na kundi la wanamgambo wa CODECO. Wakaazi hao jana walipaswa kuwasilisha kwenye ofisi ya gavana wa mkoa hotuba yao inayoelekezwa kwa Rais Tshisekedi. Lakini hawakuweza kukaidi polisi waliotawanywa kwenye maeneo mbalimbali mjini Bunia.

Ni tangu Mei 6 mwaka 2021 ndipo Rais Félix Tshisekedi aliamua kuiweka Ituri na Kivu Kaskazini chini ya utawala wa kijeshi, ili kukomesha ukosefu wa usalama na ghasia katika majimbo hayo ya Mashariki mwa nchi hii. Lakini ghasia bado zinaendelea na hali inazidi kuwa mbaya zaidi siku hadi siku.

''Hakuna mabadiliko. Waasi wanaendelea kuwauwa watu kama kawaida. Hakuna kitu ambacho jeshi limefanya kwa kusimamisha mauwaji, uporaji wa vitu na uharibifu wa vitu. Mauwaji yanaendelea hata katika kambi za wakimbizi. Kambi kadhaa zimeshambuliwa. Zaidi ya watu 62 waliuwawa. Hapa tunaendelea kulia. Hatuwaoni viongozi wanafuatilia waasi,'' alisema Dieudonné Lossa Dekhana, mratibu wa shirika la kiraia mkoani Ituri.

Wakazi wa Ituri wamemwomba Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kumuondoa gavana wa sasa wa kijeshi, Johny Luboya Nkashama ambaye shirika la kiraia linamshtumu kwa kushindwa kukomesha ghasia.

Miongoni mwa malalamiko ambayo watu wa Ituri walitaka kuyawasilisha kwa Rais Tshisekedi ambaye walitarajia atafika huko ili kuwapongeza baada ya mauaji yaliyofanywa wiki mbili zilizopita, na kujionea binafsi hali ya usalama jinsi ilivyo mkoani humo.

''Bahati mbaya, baba wa taifa hakuonekana kwa sababu ya kazi iliyomkumba. Tunaomba baba wa taifa amuondowe ndani ya siku kumi, gavana wa Ituri Johny Luboya Nkashama kwa sababu hana mpango wa kumaliza vita katika mko wa Ituri. Amteue gavana mwengine ambaye anaweza kuwa na maoni mapya kwa kumaliza vita Ituri,'' alisema Dieudonné Lossa Dekhana.

Tumejaribu kuwasiliana na gavana Johny Luboya ila hatujafanikiwa. Aidha, imeripotiwa kuwa hivi karibuni, vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, FARDC vimepelekwa Ituri ili kuwaunga mkono askari wengine ambao tayari wanapambana na wanamgambo huko.

Mwandishi: Jean Noël Ba-Mweze, DW Kinshasa.