1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza: Miili iliyoanza kuharibika yazikwa pamoja

Angela Mdungu
14 Novemba 2023

Miili iliyoanza kuharibika katika hospitali kubwa zaidi ya Ukanda wa Gaza ya Al Shifa imezikwa katika kaburi la pamoja.

https://p.dw.com/p/4YnpN
Picha ya satelaiti inayoonesha Hospitali ya Al shifa wakati mzozo wa Israel na Hamas ukiendelea
Picha ya satelaiti inayoonesha Hospitali ya Al shifa wakati mzozo wa Israel na Hamas ukiendeleaPicha: Maxar Technologies/Handout/REUTERS

Maziko hayo yamefanyika wakati Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kiutu hapo jana iliripoti kuwa kulikuwa na miili karibu 100 katika viwanja vya hospitali hiyo ambayo haikuweza kufanyiwa maziko.

Kulingana na msemaji wa  Wizara ya Afya ya Gaza iliyo chini ya kundi la Hamas, maziko ya miili 180 ya watu waliouwawa, iliyoharibika yamefanyika katika eneo la hospitali ya al Shifa. Kauli hiyo imetolewa wakati mapambano makali kati ya wanajeshi wa Israel na Hamas yakiendelea.

Soma zaidi: Vifaru vya Israel vipo kwenye milango ya hospitali ya Gaza

Katika kauli nyingine, Shirika la Afya duniani WHO limesema licha ya kukatika kwa umeme na mashambulizi yanayoendelea, wafanyakazi wake wanafanya kila liwezekanalo kuwahudumia wagonjwa takriban 700 wenye hali mbaya waliosalia hospitalini hapo. Shirika hilo limeeleza pia kuwa kati ya wagonjwa hao, 20  wamefariki dunia ndani ya saa 24 zilizopita. 

Kilio cha Waandishi Habari huko Gaza

Kutokana na mzozo unaoendelea, Shirika la Umoja wa Mataifa limesema leo kuwa huduma ya maji katika eneo la kusini la Ukanda wa Gaza zimesimama kutokana na ukosefu wa nishati.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kiutu OCHA imearifu kwamba kutokana na upungufu huo, vituo vya umma vya kuondowa majitaka, visima 60 vya maji safi katika eneo la kusini na mitambo ya kusafisha maji kwenye mji wa Rafah vyote vimesitisha huduma.

Kando ya hayo, jeshi la Israel limethibitisha leo Jumanne kifo cha mwanajeshi wake wa kike aliyekuwa akishikiliwa mateka na kundi la Hamas tangu kundi hilo lilipofanya mashambulizi  Israel Oktoba 7.

Israel yathibitisha kifo cha mwanajeshi wake aliyekuwa mateka

Awali, kundi hilo lilichapisha video ya mwanajeshi huyo Noa Marciano mwenye miaka 19 akiwa hai, na kufuatiwa na sehemu ya video iliyouonesha wili wake ukiwa na jeraha la kichwa. Msemaji wa Hamas, Abu Obeida ametanabaisha kuwa Marciano ameuwawa kutokana na mashambulizi ya Israeli.

Kifo cha mwanajeshi huyo kinaifanya idadi ya wanajeshi wa Israel waliofariki dunia kutokana na vita hivyo vinavyoendelea kufikia 47.Kadhalika Jeshi la Israel limesema leo kuwa limeyakamata majengo ya Bunge la Gaza na taasisi nyingine za serikali inayoongozwa na kundi la Hamas ndani ya Ukanda wa Gaza.

Wanajeshi wa Israel wakati wa operesheni ya ardhini Gaza
Wanajeshi wa Israel wakati wa operesheni ya ardhini GazaPicha: Israeli Defense Forces/REUTERS

Kwingineko, msemaji wa Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu ICRC Fatima Sator akiwa mjini Geneva amesema  kuwa kamati hiyo inafanya mazungumzo na kundi la Hamas ili kuwafikia mateka lililowakamata kutoka Israel. Sator amesema iwapo wafanyakazi wa kamati hiyo hawatoruhusiwa kuwaona mateka hao, wanapaswa walau kuruhusiwa kuwatumia dawa na kuhakikisha kuwa wanaweza kuwasiliana na familia zao.

Msemaji wa kamati hiyo ya msalaba mwekundu amesisitiza kuwa shirika hilo haliegemei upande wowote na kuwa siku zote linategemea makubaliano na pande zinazohusika na mzozo. Shirika la msalaba mwekundu limewezesha kurejeshwa kwa baadhi ya mateka kupitia makubaliano ya aina hiyo.