1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Miili 400 yagunduliwa Kherson, Ukraine

14 Novemba 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema leo kwamba nchi yake iko tayari kwa mazungumzo ya amani huku akiyashukuru mataifa yote na hususan ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO kwa kuisaidia Ukraine.

https://p.dw.com/p/4JTgA
Ukrainie | Präsident Selenskyj
Picha: Ukrainian Presidency/abaca/picture alliance

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema alipozuru mkoa wa Kherson kwamba anayashukuru mno mataifa yote kwa msaada mkubwa na sasa wako tayari kwa amani. Mapema, Ukraine ilisema wachunguzi katika mkoa huo wamegundua visa zaidi ya 400 vya uhalifu wa kivita vilivyofanywa na wanajeshi wa Urusi. 

Zelenskiy amesema katika hotuba yake ambayo huitoa kila usiku kwamba kumegunduliwa uhalifu mbaya uliofanywa na wanajeshi hao wa Urusi ambao wamejiondoa kwenye mkoa huo wa Kherson mwishoni mwa wiki iliyopita. Kulingana na kiongozi huyo, kumegunduliwa miili ya raia na wanajeshi wa Ukraine katika mkoa huo wa Kherson.

Alisema, ''Wachunguzi tayari wamerekodi zaidi ya visa 400 vya uhalifu wa kivita uliofanywa na Urusi. Miili ya raia na wanajeshi imepatikana. Katika mkoa wa Kherson, jeshi la Urusi lilifanya uhalifu kama ilivyofanya katika mikoa mingine ya nchi yetu, ambapo ilifanikiwa kuvamia. Tutahakikisha tunampata kila muuaji na kumfikisha mbele ya haki bila shaka yoyote.''

Soma Zaidi:Ukraine yachukua udhibiti wa mji wa Kherson 

Ingawa baadhi ya wanajeshi wa Urusi bado wangali kwenye eneo hilo, jeshi la Ukraine limeripoti kuirejesha baadhi ya miji pamoja na mji mkuu wa mkoa huo.

Bundeskanzler Olaf Scholz (SPD) reist nach Asien
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema ni aibu kwa rais Vladimir Putin kushindwa kuhudhuria mkutano wa G20 ili kuyajibu masuala dhidi ya hatua yake ya kuivamia Ukraine. Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Baadhi ya viongozi wa mataifa ya Magharibi wameshutumu uhalifu huo wa kivita uliofanywa na Urusi baada ya kushuhudia uharibifu kwenye mikoa ya Ukraine na hasa baada ya Urusi kuondoka kwenye maeneo hayo. Maafisa wa Ukraine pia wamefichua kuhusu makaburi ya pamoja katika maeneo hayo.

Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu, ICCkwa sasa inachunguza uwezekano wa uhalifu wa kivita.

Waziri wa Fedha wa Marekani Janeth Yellen, amesema kabla ya mkutano wa kundi la nchi zilizoendelea na zile zinazoinukia kiviwanda G20 huko Bali, Indonesia kwamba hakuna namna bora zaidi juu ya mgogoro huo wa Ukraine, zaidi ya kumaliza mapigano, ili pamoja na mambo mengine kuunusuru uchumi wa ulimwengu.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kwa upande wake amesema ni aibu kubwa kwa rais wa Urusi, Vladimir Putin kutohudhuria mkutano huo. Akizungumza akiwa Hanoi huko Vietnam, Scholz amesema Putin alitakiwa kufika ili apambane na ukosoaji wa ana kwa ana wa vita alivyovianzisha. Putin alsema hatashiriki siku chache zilizopita na sasa atawakilishwa na waziri wa mambo ya nje, Sergei Lavrov.

Mkutano huo wa kilele wa siku mbili wa G20 unaanza kesho Jumanne na Rais Zelenskiy atahutubia kwa njia ya video.

Soma Zaidi: Ukraine yataja masharti ya kufanya mazungumzo na Moscow

Mashirika: DW