1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 90 ya gazeti ya Kijerumani nchini Namibia

Dagmar Wittek / Maja Dreyer24 Julai 2006

azeti lililopo kwa muda mrefu zaidi barani Afrika ni gazeti la kila siku la Kijerumani linalochapishwa nchini Namibia ambayo zamani ilikuwa koloni ya Kijerumani. Hivi juzi gazeti hili limesheherekea miaka 90 tangu lianzishwe.

https://p.dw.com/p/CHmu
Wanamibia wengi wana asili ya Kijerumani
Wanamibia wengi wana asili ya KijerumaniPicha: AP

Tangu mwaka 1916 gazeti hili linawafahamisha Wanamibia wanaoongea Kijerumani juu ya matukio ya kisiasa, kijamii, kiuchumi au sanaa. Hasa kwa Wanamibia wa asili ya Kijerumani gazeti hili la “Allgemeine Zeitung” lina umuhimu maalum.

Wanamibia wa asili ya Kijerumani wanalipenda gazeti hili linalochapishwa katika lugha yao ya mama. Pia linasaidia kuwajumuisha wananchi na ni chombo cha kubadilishana habari, kama Mnamibia mmoja anavyoeleza: “Ni kweli, gazeti la “Allgemeine Zeitung” ni muhimu sana kwa sisi jamii ya Kijerumani. Kwa mfano, matangazo ya vifo au kuzaliwa kwa mtoto. Tunasema, ala, angalia hapa, wale wameoana ama huyu amekufa.”

Almute Öl ni mtangazaji wa muda mrefu wa redio ya Kijerumani nchini Namibia. Naye anasema: chai ya asubuhi bila ya gazeti hili haiwezekani. Yeye analisoma tangu alipokuwa mtoto: “Sitaki kuwa bila ya gazeti la “Allgemeine Zeitung” kwani linaunganisha nchi yetu. Halafu gazeti hilolinataja masuala ambayo hayapo kwenye magazeti mengine, hasa kutoka jamii ya Kijerumani. Tunajivunia kuwa na gazeti hilo na ninalinunua kila siku.”

Kila siku gazeti lina karasa 12 hadi 16. Lakini halihusu tu masuala ya Kijerumani, wala si gazeti la watu waliobaki nyuma. Mwandishi mkuu, Stephan Fischer, anapinga vikali kukosolewa hivyo:
“Kile kilicho cha Kijerumani ni lugha tu! Si gazeti la Ujerumani nchini Namibia, kama watalii wengi wanavyoamini. Bali ni gazeti la Namibia na lugha tu ni Kijerumani.”

Mada zilizopo ni marekebisho ya umilikaji mashamba, uhalifu, matokeo ya hali ya hewa, kama mvua au joto jingi mno na bila shaka siasa na vita dhidi ya rushwa. Kwa hivyo, masuala mengi yanahusu Namibia kwa jumla.

Mwandishi wa habari Doro Greve anataka kupunguza zaidi habari zinazohusu jamii ya Kijerumani tu. Anasema: "Mara kwa mara nadhani, wasomaji wetu wamebaki katika miaka ya 80, na sisi tuna jukumu la kuwapeleka wasomaji hawa kwenye wakati wa sasa na kuwaambia: Hey, angalia, hiyo ndiyo Namibia, ni mpya sasa! Njoo basi ushiriki. Tumeona kwamba Wajerumani zaidi wanakaa kimya katika majadiliano ya kitaifa.”

Kwa hivyo, lengo la gazeti siyo kufahamisha wasomaji wake bali pia kuwajumuisha katika jamii ya kisasa.