1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia 100 wamekwama kwenye kiwanda cha Azovstal

10 Mei 2022

Meya wa mji wa Mariupol amesema, takribani raia 100 bado wamekwama kwenye kiwanda cha chuma cha Azovstal, ambacho kinakabiliwa na mashambulizi makali kutoka kwa vikosi vya Urusi.

https://p.dw.com/p/4B55T
Ukraine | Evakuierte aus dem Azovstal Stahlwerk
Picha: ALEXANDER ERMOCHENKO/REUTERS

Msaidizi wa Meya wa Mariupol Petro Andryushchenko amesema Jumanne kuwa raia wapatao 100 bado wamebaki kwenye kiwanda hicho kilichopo kwenye mji huo wa bandari. Hata hivyo, Petro ameandika katika mtandao wa mawasiliano wa Telegram kuwa hali hiyo haipunguzi mashambulizi yanayofanywa na Urusi. Awali Ukraine ilisema raia wote wameondoka kwenye kiwanda cha Azovstal na Urusi pia ilidai kuwa zoezi la kuwaondoa raia kutoka kwenye eneo hilo, limekamilika.

Miili 44 ya raia imekutwa kwenye kifusi

Hayo yanajiri wakati ambapo afisa mmoja wa Ukraine amesema miili ya raia 44 imekutwa katika kifusi kwenye jengo moja katika eneo la Izyum, lililoko katika mji wa Kharkiv ambao umeharibiwa na Urusi mwezi Machi.

Afisa huyo, Oleh Synehubov ameandika katika mtandao wa Telegram kwamba jengo hilo la ghorofa tano lilianguka likiwa na watu ndani. Kwa mujibu wa Oleh, huo ni uhalifu mwingine wa kivita wa kutisha dhidi ya raia uliofanywa na Urusi inayoikalia kimabavu Ukraine.

Ama kwa upande mwingine, jeshi la Ukraine limesema Jumanne kuwa majeshi ya Urusi yamefyatua makombora saba jana usiku kuelekea kwenye mji wa bandari wa Odesa ulioko kusini mwa Ukraine. Kituo cha maduka makubwa na bohari moja vimeshambuliwa na kusababisha mauaji ya mtu mmoja na wengine watano kujeruhiwa.

Nächtliche Luftangriffe an Odesa
Eneo la maduka mjini Odesa lililoshambuliwa na makombora ya UrusiPicha: Oleksandr Gimanov/AFP

Msemaji wa jeshi, Natalya Gumenyuk ameandika katika mtandao wa Facebook kwamba, wakati wa kutafuta malengo ya kimkakati, makombora yamefanikiwa kuyaharibu maeneo hayo.

Marekani: kuna dalili raia wa Ukraine wanapelekwa Urusi kwa lazima

Wakati huo huo, Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema kuna dalili zinazoonesha kuwa raia wa Ukraine wanapelekwa kwa nguvu nchini Urusi. Msemaji wa wizara hiyo, John Kirby Jumatatu aliwaambia waandishi habari kwamba raia wa Ukraine wanachukuliwa bila ridhaa yao na kupelekwa Urusi.

''Siwezi kusema idadi ya watu wangapi ambayo tumeiona, lakini kwa hakika tumeona dalili kwamba raia wa Ukraine wanapelekwa Urusi. Dalili nyingine ni kwamba Urusi haitoukubali na kuuheshimu uhuru wa watu wa Ukraine na kwamba wao ni raia wa taifa jingine,'' alifafanua Kirby. Kirby ameitoa kauli hiyo kujibu madai ya Ukraine kwamba takribani watu milioni 1.2 wamepelekwa Urusi na wamewekwa kwenye kambi mbalimbali.

USA Washington | Pentagon-Sprecher John Kirby
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, John KirbyPicha: Andrew Harnik/AP/dpa/picture alliance

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock Jumanne anatarajiwa kuizuru Ukraine, ziara inayotarajiwa kusaidia kuimarisha uhusiano baada ya kuwepo mvutano wa kidiplomasia kuhusu upelekaji wa silaha.

Makubaliano ya marufuku ya mafuta kufikiwa karibuni

Aidha, Waziri wa Ufaransa anayeshughulikia masuala ya Umoja wa Ulaya, Clement Beaune, amesema nchi wanachama za umoja huo zinakaribia kufikia makubaliano madhubuti kuhusu pendekezo la umoja huo la kupiga marufuku uagizaji wa mafuta kutoka Urusi.

Nalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana kwa mara nyingine tena siku ya Alhamisi kuujadili uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Hiki kitakuwa kikao cha 16 tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake Februari 24.

Mkutano wa sasa unafanyika kutokana na maombi ya Ufaransa na Mexico. Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa litakutana Alhamisi kuzungumzia kuzorota kwa hali ya haki za binaadamu nchini Ukraine.

(AP, AFP, Reuters DW https://bit.ly/3MdCPxW)