1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya mkataba wa nyuklia na Iran mbioni kuanza tena

25 Juni 2022

Iran imeahidi kuwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati yake na Marekani ya kuufufua mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 yatarejea tena hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/4DEy9
Iran | Treffen Josep Borrell und Hossein Amir Abdollahian in Teheran
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell (kushoto) alipokutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Hossein Abdollahian mjini Tehran.Picha: Fatemeh Bahrami/AA/picture alliance

Hayo yamesemwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Hossein Amirabdollahian baada ya kukutana na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell aliyeitembela Iran siku ya Jumamosi.

Ziara ya Borell inalenga kusukuma juhudi za kumaliza mkwamo unaoyakabili majadiliano yaliyositishwa ya mjini Vienna ambayo yanajadili uwezekano wa kuufufua mkataba huo wa nyuklia kati ya Iran na madola yenye nguvu duniani.

"Tumejitayarisha kurejea kwenye mazungumzo katika siku zinazokuja. Kile kilicho muhimu kwa Iran ni kupatiwa nafuu za kiuchumi zilizoanishwa chini ya mkataba wa mwaka 2015" amekaririwa akisema waziri Hossein Amirabdollahian na kuongeza kuwa mazungumzo yake na Borell yalikuwa marefu lakini yenye manufaa.

Wajumbe kujaribu kutanzua mkwamo uliopo

Iran | Treffen Josep Borrell und Hossein Amir Abdollahian in Teheran
Picha: Fatemeh Bahrami/AA/picture alliance

Pande zinazojadiliana zilikuwa karibu kufikia makubaliano ya kuufufua mkataba huo mnamo mwezi Machi.

Wakati huo Umoja wa Ulaya ambao ndiyo unaratibu mazungumzo hayo uliwaalika mawaziri wa mambo ya kigeni wa pande zinazohusika mjini Vienna kukamilisha makubaliano baada ya miezi 11 ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na utawala wa rais Joe Biden wa Marekani.

Hata hivyo mazungumzo hayo yaliingia kiwingu baada ya tehran kushinikiza kwanza Marekani itakangaze kukiondoa kikosi cha walinzi wa mapinduzi cha jeshi la Iran kwenye orodha yake ya makundi ya kigaidi.

"Tunatarajia kurejea mezani hivi karibuni na kumaliza mkwamo uliopo. Miezi mitatu imepita na sasa yatupasa kuharakisha kazi. Nimefurahi kwa uamuzi ambao umefikiwa kati ya Tehran na Washington" amesema Borell alipokuwa akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran.

Borell asema mazungumzo yataanza bila kuchelewa 

Atomanlage im Iran
Picha: Getty Images

Maafisa wawili, mmoja kutoka Iran na mwingine kutoka barani Ulaya waliliambia shirika la habari la Reuters kabla ya ziara ya Borell mjini Tehran kwamba "masuala mawili ikiwemo moja la vikwazo vya kiuchumi bado hayajapatiwa ufumbuzi".

Taarifa hiyo haijathibitishwa wala kukanushwa na wizara ya mambo ya kigeni ya Iran.

Baadae Borell aliandika kupitia ukurasa wa Twitter kwamba wamekubaliana juu ya kurejea kwa mazungumzo kati ya Iran na Marekani katika siku chache zinazokuja chini ya usimamizi wa Umoja wa Ulaya ili kutatua vizingiti vilivyosalia.

Hata hivyo hakueleza ni wapi majadiliano hayo yatafanyika.

Amesisitiza makubaliano hayo yanamaanisha mazungumzo kati ya pande hizo yatafanyika haraka iwezekanavyo bila kupoteza muda.

Mparaganyiko ni sehemu ya urathi wa utawala wa rais wa zamani wa Marekani 

Atomanlage im Iran
Picha: Getty Images

Mnamo mwaka 2018, rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump aliiondoa nchi yake kutoka mkataba wa nyuklia na Iran ambao ulifikiwa mwaka 2015 kwa sharti kwamba dola hiyo ya Uajemi ipunguze shughuli zake za nyuklia kwa ahadi ya kupunguziwa vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa na mataifa ya magharibi hususani Marekani.

Kujiondoa huko kwa Marekani na kurejeshwa kwa vikwazo vyake vya kiuchumi kuilighadhibisha Iran ambayo ilianza kupuuza utekelezaji wa masharti ya mkataba huo wa nyuklia ikiwemo kuongeza kiwango cha urutubishaji wa madini ya Urani.

Madola ya magharibi yanashuku kuwa Iran inakaribia kufikia uwezo wa kuunda bomu la nyuklia lakini Jamhuri hiyo ya kiislamu inakanusha madai hayo ikisema mradi wake wa nyuklia ni kwa matumizi salama na siyo kijeshi.