1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yasema haina nia ya kumiliki silaha za nyuklia

17 Februari 2022

Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameapa kwamba nchi yake itaendeleza mpango wake wa nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani, akionya kwamba hawana nia ya kumiliki silaha za atomiki

https://p.dw.com/p/47BeM
Iran, Tehran I Ayatollah Ali Khamenei
Picha: Office of the Iranian Supreme Leader/AP/picture alliance

Katika hotuba aliyoitoa moja kwa moja kupitia runinga ya taifa, Ayatollah Ali Khamenei amehimiza umuhimu wa nishati ya nyuklia kwa taifa lake, akisisitiza kuwa Iran haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia. Matamshi ya Khamenei  yanaonekana kuyalenga mataifa yaliokusanyika mjini Vienna kwa mazungmzo kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Khamenei ameongeza kwamba maadui wa Jamhuri hiyo ya kiislamu wanachukua hatua dhidi ya mpango wake wa nishati ya nyuklia na kuweka vikwazo juu ya nishati hiyo wanayojua ni kwa matumizi ya amani akisema maadui hao hawataki kuiona Iran ikifikia malengo yake.

Iran ipo katika mazungumzo ya nyuklia pamoja na mataifa yalio na nguvu kujaribu kuufufua mkataba wa nyuklia uliotiwa saini mwaka 2015 na kufungua nafasi ya taifa hilo kufutiwa vikwazo vya kiucumi ilivyowekewa, ili iachane na mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia, mpango ambao Iran imeendelea kukanusha.

Ali Bagheri asema huenda wakafikia makubaliano karibuni

Österreich | Atomgespräche mit dem Iran
Mjumbe Mkuu wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran Ali Bagheri, akiwa pamoja na wajumbe wengine Picha: Joe Klamar/AFP

Huku hayo yakiarifiwa Mjumbe Mkuu wa Iran katika mazungumzo hayo ya mjini Vienna Ali Bagheri alisema jana kuwa pande zinazoshiriki zipo karibu kufikia makubaliano ya pamoja.

Aliyasema hayo saa kadhaa baada ya Ufaransa kuonya kuwa Iran imebakisha siku chache kukubaliana na matakwa ya mataifa yaliyo na nguvu ambayo ni Marekani, Urusi, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.

Mazungumzo hayo hayajafanikiwa kwa mara kadhaa katika miezi ya hivi karibuni kufuatia wapatanishi wa Iran kutoa matakwa magumu yaliyowakasirisha wanadiplomasia wa Magharibi.

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, alijiondoa takriban miaka 4 iliyopita, katika makubaliano hayo ya nyuklia kati ya Iran na mataifa yalio na nguvu duniani, Hatua hii pia iliilaazimu Iran kurutubisha urani kwa viwango vya juu kabisa vilivyofikia asilimia 60 ikiwa ni hatua chache tu iliyobakia ya asilimia 90 inayohitajika kurutubishwa kufikia viwango vinavyohitajika kutengeneza mabomu ya atomiki na kukiuka kabisa makubaliano ya mkataba wa 2015.

Chanzo: afp/ reuters