Mazungumzo ya kusitisha vita Gaza yapiga hatua kubwa
14 Januari 2025Maafisa hata hivyo wamesema makubaliano rasmi ya kusitisha vita bado hayajafikiwa.
Maafisa wanne wamekiri kwamba kumepigwa hatua na kuongeza kuwa siku zijazo zitakuwa na umuhimu mkubwa kuelekea kupatikana kwa makubaliano ya kusitisha vita vya zaidi ya miezi 15 ambavyo vimevuruga eneo la Mashariki ya Kati.
Maafisa hao wamezungumza kwa masharti ya kutotajwa majina kwa sababu hawajaruhusiwa kujadili kuhusu mazungumzo hayo yanayofanyika mjini Doha, Qatar.
Soma pia: Duru mpya ya mazungumzo kuhusu mzozo wa Gaza
Afisa mmoja wa Marekani anayefahamu kwa undani juu ya mazungumzo hayo amesema, pande zote ziko karibu zaidi kufikia makubaliano, lakini ametahadharisha kuwa bado hali inaweka kubadilika wakati wowote.
Bado kuna vipengele vinavyohitaji kupigwa msasa
Afisa huyo amekataa kutoa utabiri juu ya wakati ambao makubaliano hayo yanaweza kufikiwa akisema kuna hali isiyoeleweka, na vipengele vingi bado havijakamilika.
Maafisa wengine wawili, akiwemo mmoja anayehusishwa na Hamas, wamesema bado kuna vikwazo kadhaa. Mara kadhaa katika kipindi cha mwaka uliopita, viongozi wa Marekani walieleza matumaini kwamba, walikuwa karibu kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano, ingawa baadaye mazungumzo hayo yalikwama.
Afisa mwengine mwenye ufahamu juu ya suala hilo, amefahamisha kwamba kumekuwepo dalili ya kufikia makubaliano na tayari lipo pendekezo kwenye meza ya mazungumzo.
Inaripotiwa kuwa, wajumbe wa Israel na Hamas wataliwasilisha pendekezo hilo kwa viongozi wao kwa ajili ya idhini ya mwisho.
Soma pia: Mkuu wa ujasusi wa Israel kujadili usitishaji vita Gaza
Afisa huyo ameendelea kueleza kwamba, wapatanishi kutoka Qatar wameweka shinikizo jipya kwa Hamas kukubali pendekezo hilo la kusitisha mapigano huku mjumbe wa Rais mteule wa Marekani Donald Trump, Steve Witkoff, kwa upande wake akiishinikiza Israel kulikubali pendekezo hilo.
Witkoff hivi karibuni alijiunga na mazungumzo hayo na ameonekana katika eneo la Mashariki ya Kati mara kwa mara katika siku za hivi karibuni.
Mjumbe wa Rais mteule Donald Trump, Steve Witkoff yuko Doha
Afisa huyo amesema wapatanishi wamekabidhi rasimu ya makubaliano kwa kila upande huku saa 24 zijazo zikitajwa kuwa na umuhimu wa kuamua hatma ya mazungumzo hayo.
Afisa mmoja wa Misri amefahamisha pia, kumekuwepo maendeleo mazuri japo huenda ikachukua siku chache zaidi kwa makubaliano rasmi kufikiwa. Inaelezwa kwamba wapatanishi wanalenga kufikia makubaliano kabla ya kuapishwa kwa Rais Donald Trump mnamo Januari 20.
Afisa wa Hamas ambaye amezungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa sababu hakupewa idhini ya kuzungumza na vyombo vya habari, ameeleza kwamba kuna masuala kadhaa yenye utata ambayo bado yanahitaji kutatuliwa, ikiwa ni pamoja na ahadi ya Israel ya kuvimaliza vita hivyo na maelezo kuhusu kuondolewa kwa wanajeshi wa Israel katika ukanda wa Gaza na ubadilishanaji wa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina.
Kiongozi Mkuu wa Qatar, Sheikh Tamin bin Hamad Al Thani, alikutana na ujumbe wa Hamas mjini Doha pamoja na Witkoff na Brett McGurk, mshauri mkuu wa Rais Joe Biden kuhusu masuala ya Mashariki ya Kati.
Al Thani pia amezungumza kwa njia ya simu na Biden, ambaye amesisitiza umuhimu wa kufikia haraka iwezekanavyo makubaliano ya kusitisha mapigano.