1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Gaza: Duru mpya ya mazungumzo kuanza mjini Doha

15 Agosti 2024

Wapatanishi wa kimataifa wanatarajiwa kuanzisha Alhamisi duru mpya ya mazungumzo kwa lengo la kusitisha vita kati ya Israel na kundi la Hamas.

https://p.dw.com/p/4jURq
Jordan- Blinken na viongozi wa kiarabu wakijadili mzozo wa Gaza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiwa na viongozi wa Jordan, Misri, Qatar, Saudi Arabia na Mamlaka ya Palestina kujadili vita vya GazaPicha: JONATHAN ERNST/AFP

Marekani, Misri na Qatar zinatarajiwa kukutana kwa mazungumzo na wajumbe wa Israel mjini Doha katika duru hiyo mpya ya mazungumzo ambayo huenda ikawezesha kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha vita na hivyo kuleta matumaini ya kuepuka mzozo mpana zaidi wa kikanda.

Haikufahamika wazi ikiwa Hamas ingelishiriki  mazungumzo hayo   kwa kuwa wameituhumu Israel kuongeza masharti zaidi kwenye pendekezo la awali ambalo lilipendekezwa na Marekani na lililokuwa limekubaliwa na kundi hilo. Msemaji wa Hamas, Osama Hamdan ameliambia shirika la habari la AP kwamba kundi hilo linahitaji kujadili utekelezaji wa pendekezo lililotolewa na Rais wa Marekani Joe Biden, na sio kuanzisha mazungumzo mapya.

Saudi-Arabia | Antony Blinken akiwa na Al Thani mjini Riadh
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiwa na mwenzake wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani na viongozi wenginePicha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Siku ya Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani walizitolea wito Iran, Hamas na Israel kwamba hakuna upande wowote katika eneo hilo unaopaswa kuchukua hatua ambazo zinaweza kudhoofisha juhudi za kufikia makubaliano hayo.

Soma pia: Iran haitoishambulia Israel iwapo tu kutafikiwa usitishwaji mapigano Gaza

Ndugu za mateka wameandamana leo mjini Tel-Aviv wakiishinikiza serikali yao ya Israel kuafiki mpango huo. Zahiro Shahar Mor, ni mpwa wa mateka wa Israel Avraham Munder.

"Tunahitaji usitishaji mapigano ili kuwarejesha mateka wote. Hatuwezi kuiamini tena serikali ya Israel. Kwa muda wa miezi kumi iliyopita, imekuwa ikizuia juhudi zozote za kufikiwa makubaliano. Tunafahamu kuna mkutano wa kilele leo, tuna matumaini kidogo juu ya utayari wa wajumbe wa Israel kusaini makubaliano hayo. Na tunatoa wito kwa mataifa yote duniani, yatusaidie kuirekebisha hali hii."

Shinikizo na matumaini kwa mpango huo

Kusitishwa kwa mapigano huko Gaza kunaweza kusaidia kutuliza hali ya wasiwasi inayotanda katika eneo la  Mashariki ya Kati . Wanadiplomasia wanatumai kuwa kufikiwa kwa makubaliano hayo kutaishawishi Iran na kundi la Hezbollah la Lebanon kuachana na dhamira yao ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel kufuatia mauaji ya kamanda mkuu wa Hezbollah Fuad Shukur mjini Beirut na kiongozi mkuu wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh huko Tehran.

Wapalestina wakishuhudia uharibifu baada ya mashambulizi ya Israel huko Gaza
Wapalestina wakishuhudia uharibifu baada ya mashambulizi ya Israel huko GazaPicha: Ahmad Hasaballah/Getty Images

Mpango huo wa awamu tatu ungelihusisha usitishwaji mapigano Gaza, kuachiliwa kwa mateka wa Israel pamoja na wafungwa wa Kipalestina. Wakati juhudi hizo za kimataifa zikiendelea, idadi ya vifo vya Wapalestina katika mzozo huu ambao umedumu kwa miezi kumi sasa, inakaribia kufikia watu 40,000, hii ikiwa ni kulingana na mamlaka za afya huko Gaza zinazodhibitiwa na Hamas.

Soma pia: Amnesty: Israel ikomeshe mateso kwa Wapalestina Gaza

Katika hatua nyingine, Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas anatarajiwa kulihutubia bunge la Uturuki katika mji mkuu Ankara leo Alhamisi, siku moja baada ya kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin mjini Moscow. Siku ya Jumatano, Abbas alikutana na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan na kuzungumzia kuhusu vita vya Gaza na hatua zinazohitajika kuchukuliwa ili kufikia mpango wa kudumu wa usitishwaji mapigano.

Vyanzo: (AFP, AP, Reuters, DPAE)