1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya wakutana Estonia

8 Septemba 2017

Mawaziri wa ulinzi wa nchi za Umoja wa Ulaya wamesema wana imani kwamba kufikia mwishoni mwa mwaka huu nchi zao zitaanzisha ushirikiano wa ulinzi wa bara la Ulaya hivyo kufanikisha kupatikana suluhisho la kudumu.

https://p.dw.com/p/2jb85
Estland Treffen der EU-Verteidigungs- und Außenminister | Federica Mogherini, EU-Außenbeauftragte
Picha: Getty Images/AFP/R. Pajula

Mawaziri hao wamekutana mjini Tallinn huko nchini Estonia. Nchi hiyo hiyo ndio kwa sasa inayoshikilia uenyekiti wa mzunguko wa Umoja wa Ulaya. Chini ya mpango huo wa ulinzi nchi za Umoja wa Ulaya zinapanga kuanzisha mpango utakaogharimu mabilioni ya Euro ambapo nchi zote husika zitachangia. Waziri wa ulinzi wa Estonia Juri Luik amesema ni muhimu kwa fedha hizo zinazochangwa na nchi husika kuwa zitaimarisha ulinzi wa nchi za Ulaya. Waziri Luik amesema fedha zinazochangwa kwa ajili ya utafiti na maendeleo bila shaka zitaimarisha ulinzi wa bara Ulaya na kwamba nchi za Ulaya zitafanikiwa kuendeleza mipango ya ushirikiano ya kudumu na wakati huo huo kuutunisha mfuko wa ulinzi wa nchi za Ulaya hadi kufikia mwisho wa uenyekiti unaozunguka wa nchi za Umoja wa Ulaya.

Estland Treffen der EU-Verteidigungs- und Außenminister in Tallinn
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der LyenPicha: Getty Images/AFP/R. Pajula

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen ameelezea maendeleo yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka mmoja uliopita. Kwa mujibu wa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini mawaziri wa ulinzi pia walikubaliana kuongeza uwepo wa nchi hizo katika eneo la Sahel na pembe ya Afrika ili kupambana na makundi ya kigaidi pamoja na yale yanayoendesha shughuli za kuwasafirisha watu kinyume cha sheria. Baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa mawaziri wa ulinzi kutoka nchi za Umoja wa Ulaya nao mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo walianza mkutano wao unaotarajiwa kumalizika hii leo na moja kati ya ajenda muhimu zinazojadiliwa ni suala la Korea Kaskazini na iwapo nchi za Umoja huo zinapaswa kuiwekea Korea kaskazini vikwazo zaidi baada ya nchi hiyo kufanya jaribio jingine la kombora.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/RTRE

Mhariri:Saumu Yusuf