1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kuwawekea vikwazo viongozi waasi wa Niger

31 Agosti 2023

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya wanaokutana nchini Uhispania wamesisitiza umuhimu wa demokrasia, wanajadili pia juu ya jumuiya ya Umoja wa Ulaya katika kuiunga mkono Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi.

https://p.dw.com/p/4VoLQ
Spanien Toledo | Treffen der EU Außenminister
Picha: Andrea Comas/AP/picture alliance

Mawaziri hao vilevile wanatafakari juu ya kuiwekea vikwazo serikali ya Niger na kuyachunguza mashirika yanayoiunga mkono serikali hiyo ya kijeshi.

Hatua hiyo ni baada ya Ujerumani na Ufaransa kupendekeza hayo na pia pendekezo sawa na hilo kutolewa na mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell.

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytri Kuleba naye yupo nchini Uhispania kuhudhuria mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya katika mji wa Toledo.

Alipowahutubia mawaziri, Kuleba alisema nchi yake haihitaji tu silaha zaidi kwa ajili ya vita vinavyoendelea, lakini pia inahitaji magari ya wagonjwa yanayotumika vitani ili kuwaondoa wanajeshi waliojeruhiwa.

Kwingineko kabla ya Mkutano Mkuu wa 78 wa Umoja wa Mataifa na mkutano wa mataifa wanachama wa G20 utakaofanyika nchini India.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameisifu hatua ya kimataifa iliyosaidia katika kuunda mpango wa amani wa Ukraine.

Hata hivyo Bearbock ameeleza wasiwasi wa Ukraine na washirika wake kutokana na kwamba India haikumwalika Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwenye mkutano huo wa kilele wa kundi la G20.

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya umepinga hatua ya kunyakua madaraka kwa nguvu nchini Gabon na umetoa wito kwa pande zote kujizuia.

Mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo Josep Borrell ameyasema hayo katika taarifa yake ya leo Alhamisi.

Borrell amesema changamoto zinazoikabili Gabon lazima zitatuliwe kwa mujibu wa kanuni za kisheria, utaratibu wa kikatiba na demokrasia.

Amesema amani ya nchi hiyo, ustawi, pamoja na utulivu wa kikanda, zinaitegemea Gabon. Mapema leo, Borrell aliwaambia waandishi wa Habari kwamba uchaguzi wa Gabon ulikumbwa na kasoro.