1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJapan

Mawaziri wa G7 waahidi kuwakabili washirika wa Urusi

18 Aprili 2023

Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa kundi la nchi tajiri za G7 wamekamilisha mkutano wao wa siku mbili nchini Japan kwa kutoa onyo kwa wale wanaoisaidia Urusi kuendelea na vita vya Ukraine wakisema "watalipa gharama kubwa".

https://p.dw.com/p/4QEMg
Japan | Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa kundi la G7.
Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa Mataifa ya kundi la G7 na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya wakiwa kwenye mkutano nchini Japan.Picha: Yuichi Yamazaki/REUTERS

Wanadiplomasia hao waliokuwa wakikutana tangu siku ya Jumapili kwenye mji wa mapumziko wa Karuizawa, wamemaliza mkutano wao kwa maazimio ya kutafuta njia za kuizuia Urusi kuendelea na vita nchini Ukraine.

Ijapokuwa hawajatangaza vikwazo vipya dhidi ya Moscow mawaziri hao wa Marekani, Canada, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Japan na Italia wameahidi kuwadhibiti wote wanaoisaidia Urusi kukwepa vikwazo vikali vya kiuchumi vilivyoweka na mataifa ya magharibi.

Hilo linajumuisha vilevile wale wanaoiwezesha Moscow kupata silaha za kupigana nchini Ukraine.

Kwenye mkutano na waandishi habari waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken pia aliituhumu Urusi kuzuia usafirishaji nafaka ya Ukraine akisema mwenendo huo unakiuka ahadi za Moscow kwa mataifa yanayotegemea chakula na mahitaji mengine kutoka Ukraine.

Taiwan yajadiliwa lakini China haijafurahishwa 

Japan | Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa Mataifa ya kundi la G7
Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa Mataifa ya kundi la G7 na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya wakiwa kwenye mkutano nchini Japan.Picha: Andrew Harnik/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Suala jingine kubwa lililojadiliwa ni mkakati wa pamoja wa kuikabili China, ambayo kutanuka kwa nguvu zake za kijeshi na kiuchumi kumegeuka kitisho kwa washirika wa Marekani kwenye kanda ya bahari ya Hindi na Pasifiki.

Mawaziri wa kundi la G7 wameinyooshea kidole China kutokana na kuongeza shughuli zake za kijeshi kwenye bahari ya kusini mwa China inayozozaniwa.

Kadhalika suala la hadhi ya kisiwa cha Taiwan nalo limejitokeza ambapo wamesema sera ya kundi hilo kuhusu Taiwan ambayo China inadai kuwa sehemu ya milki yake, haijabadilika.

Maazimio hayo ya G7 kuhusu China, hayajapokelewa vizuri mjini Beijing. China imelaani mazungumzo ya maazimio ya mawaziri huo ikisema walitumia mkutano nchini Japan kukosoa sera kadhaa za Beijing kwa malengo ya "kuipaka matope na kuchafua jina la China”

Mzozo wa Sudan na vizuizi dhidi ya wanawake Afghanistan vyatolewa maazimio

Ingawa mazungumzo ya Karuizawa yalitawaliwa zaidi na mzozo wa Ukraine na changamoto za kikanda, ikiwemo takwa la kuishinikiza Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa makombora ya masafa marefu, wanadiplomaisa wa G7 waligusia vilivile ajenda nyingine za ulimwengu.

Mkutano wao ulifanyika katikata mwa mzozo unaotanuka nchini Sudan ambako majenerali wawili wa jeshi wanawania udhibiti wa taifa hilo. Mawaziri wa G7 wametoa mwito wa kukomeshwa uhasama nchini humo na kila upande usaidie kurejesha utulivu bila masharti yoyote.

Wapiganaji katika mzozo wa Sudan
Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa Mataifa ya kundi la G7 wametoa mwito wa kukomeshwa mapigano nchini SudanPicha: AFP

Kulikuwa na tamko pia juu ya hali nchini Afghanistan, ambapo mawaziri hao wamekosoa ongezeko la vizuizi dhidi ya haki za wanawake na makundi ya jamii za wachache.

Wamezirai mamlaka za Taliban kuondoa mara moja vizuizi vyote vipya ikiwemo tangazo linalowazuia wanawake kufanya kazi na masharika ya Umoja wa Mataifa.

Mkutano huo wa mawaziri unafungua njia kuelekea mkutano w akilele wa viongozi wa mataifa ya kundi la G7 utakaofanyika huko Hiroshima mnamo mwezi Mei.

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida anapanga kulipa umuhimu wa juu suala la kuondoa silaha za nyuklia duniani wakati wa mkutano huo.