1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya Floyd yakumbushia ubaguzi wa watu weusi Ulaya

2 Juni 2020

Hakuna ahueni kwangu kwamba naishi Ujerumani, ameandika mwandishi wa DW Chimponda Chimbelu, kuhusu mwitikio wa Ulaya juu ya mauaji ya George Floyd. Ni wakati kwa Ulaya kutafakari juu ya ubaguzi wake yenyewe, ameongeza.

https://p.dw.com/p/3d8if
Deutschland Protest nach dem Tod von George Floyd in Berlin
Picha: picture-alliance/NurPhoto/O. Messinger

Mauaji ya George Floyd yumkini ndiyo mara pekee ambapo marafiki na jamaa zangu kadhaa wameniandikia kuhusu mauaji ya kibaguzi. Baadhi wanaelezea hisia zao, na wengine wameandika kusema wapo kwa ajili yangu. Ujumbe mmoja ulikuwa mashuhuri hasa. Rafiki yangu Mjerumani aliniuliza, una furaha kwamba huishi Marekani kwa sasa? Matukio ya hivi karibuni yanahuzunisha sana," aliongeza.

Ilinichukuwa siku nzima kujibu. Hakuna ahueni kwangu kwamba naishi Ujerumani. Nimehuzunika na kuvunjwa moyo. Kwa miaka kadhaa, wanaume na wanawake weusi wameuawa, hata na polisi, kwa kuwa tu weusi. Kwetu, mauaji ya George Floyd ni ukumbusho kwamba vurugu za kibaguzi baadhi ya wakati zinasababisha kifo.

Maandamano katika miji ya Marekani, na sasa hata katika baadhi ya miji mikuu barani Ulaya, yanahusu hasa ukataji tamaa wanaohisi watu weusi kutokana na ubaguzi wa kimfumo na kitaasisi. Tusidanganyane kwamba hili ni tatizo la Marekani pekee. Ubaguzi dhidi ya watu weusi umeenea katika mataifa magharibi.

Mwaka 2011 maandamano yalifanyika mjini London baada ya Mark Duggan, mwanamume mweusi, kupigwa risasi na kuuawa na polisi.

Nchini Ufaransa, mandamano na vurugu vilizuka kufuatia vifo vya vijana wawili mwaka 2005; Bouna Traore na Zyed Benna walipigwa na umeme katika kituo cha treni cha chini ya radhi walipojaribu kuikwepa polisi, wakati kijana wa tatu, Muhittin Altun, alipata majeraha makubwa ya moto lakini alipona.

Mwaka huo huo, Oury Jallon, muomba hifadhi kutoka Sierra Leon, alikufa katika tukio la moto akiwa kizuwizi cha polisi mjini Dessau, nchini Ujerumani.   

Griechenland Athen | Polizeigewalt | Proteste gegen Rassismus
Wafuasi wa chama cha kikomunisti cha Ugiriki wakionesha mshikamano na waandamanaji wa Marekani huku wakitengeneza neno la "siwezi kupumua" nje ya ubalozi wa Marekani mjini Athens.Picha: Reuters/A. Konstantinidis

Inaweza kuwa rahisi kwa baadhi ya watu wa Ulaya kuyatazama matukio ya nchini Marekani na kusema hayo hayatokei hapa, lakini raia weusi wa Ulaya hawana fahari hiyo.

Kwao, ubaguzi wa rangi uko hai sana barani Ulaya, licha ya ukweli kwamba vurugu mikononi mwa polisi zinaweza zisionekane mara kwa mra katika taarifa za habari.

Hiyo ndiyo sababu moja mauaji ya Geroge Floyd yamesababisha maandamano makubwa mbali ya Marekani; matukio ya huko yanatonesha vidonda vya zamani. Mtazamo wa jamii za magharibi juu ya nini maana ya kuwa mweusi haitofautiani sana. Fikira zao zinahodhiwa kwa sehemu kubwa na matukio machache ya kihistoria.

Utumwa na ukoloni. Kwa bahati mbaya, maelezo ya vyombo vya habari na mitaala ya shule hayajafanya vya kutosha kubadilisha mtazamo wa watu kuhusu suala la rangi. Kwangu, ujumbe wa rafiki yangu akiniuliza iwapo nafuruahi kuwa nchini Ujerumani ulikuwa unaondosha ukweli juu ya ubaguzi wa kila siku katika taifa hili.

Mwaka 2017 watu weusi walitambuliwa katika Mpango wa Taifa dhidi ya Ubaguzi wa Rangi, kama mojawapo ya makundi matano ya watu walioko katika hatari kubwa ya kukabiliwa na ubaguzi.

Lakini hilo lilikuja tu baada ya shinikizo kutoka kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu uondoaji wa ubaguzi wa rangi, ambayo ilisema mara kwa mara kwamba Ujerumani ilikuwa haifanyi vya kutosha kupambana dhidi ya ubaguzi.

Hakuna data Ulaya kuhusu ubaguzi wa rangi

UK Protest nach dem Tod von George Floyd in London
Ubaguzi ni janga, ndivyo yanavyosomeka maneno kwenye bango hili na mwandamanaji mjini London, Uingereza.Picha: picture-alliance/AA/I. Tayfun Salci

Ujerumani haiko peke yake barani Ulaya. Ukosefu wa ufahamu na uelewa wa umma juu ya ubaguzi wa rangi barani humo unastajaabisha. Na ni vigumu kupata picha ya wazi juu ya namna ubaguzi huo unavyowaathiri watu wa rangi barani kwa sababu hakuna ukusanyaji wa data, ukiacha nchini Uingereza tu.

Maandamano yanayoendela nchini Marekani hayatoi muda wala eneo kwa Waulaya kusema kwamba hali hapa ni bora - itazame tu Ugiriki na namna iiivyokuwa ikiwashughulikia wakimbizi. Watu wa rangi, hasa weusi na Waafrika, mara nyingi huteseka mikononi mwa maafisa wa serikali na jamii kwa ujumla.

Hivi karibuni, mtandao wa Ulaya dhidi ya ubaguzi umesema ufuatiliaji wa watu kwa misingi ya rangi na vurugu za polisi barani humo wakati wa janga linaloendelea la covid-19, vinaziathiri zaidi jamii za wachache.

Mauaji ya George Floyd ni ukumbusho mwingine wa ubaguzi wa kitaasisi na kimfumo -- jambo ambalo Aminate Toure, nyota chipukizi mwenye asili ya Afrika katika siasa za Ujerumani, aligusia katika makala yake ya maoni kwa ajili ya jarida la Bento hivi karibuni - Pengine usipate wazo la kumwambia mtu afurahie kwamba hawajafyatuliwa risasi, aliandika.

Kwa kuwa tu hatuzungumzii juu ya vifo haimaanishi kwamba ubaguzi siyo tatizo barani Ulaya pia. Tunaweza kuonyesha mshikamano wetu kwa kumtaja George Floyd na kujadili dhulma za ubaguzi na namna unavyoathiri maisha ya watu katika jamii zetu wenyewe, ili tuweze kuuzuwia.

Chanzo: DW