1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Tumesikitishwa na shambulizi lenye madhara Gaza

29 Desemba 2023

Mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas yanaendelea kupamba moto. Serikali ya Israel imedai kusikitishwa na mashambulizi yake kwenye kambi moja ya wakimbizi ambako zaidi ya watu 70 wameuawa.

https://p.dw.com/p/4agxm
Israel | Kikosi cha ardhini cha kitengo cha makombora
Vikosi vya Israel vikiendeleza mashambulizi ya ardhini katika Ukanda wa Gaza.Picha: Ohad Zwigenberg/AP/dpa/picture alliance

Vikosi vya Israel vimeshambulia miji kadhaa na kambi za wakimbizi kote katika Ukanda wa Gaza. Mashambulio hayo ya anga na ya ardhini yaliochochewa na mashambulizi ya kundi la wanamgambo wa Hamas takriban wiki 12 zilizopita yamesababisha vifo vya watu wengi.

Mpaka sasa zaidi ya Wapalestina 20,000 wameuawa na takriban asilimia 85 ya watu milioni 2.3 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao.

Soma Pia:Wizara ya afya Gaza yasema vifo kutokana na vita na israel vimefikia 21,320

Maafisa wa Israel wameelezea juu ya shambulio la anga katika kambi ya wakimbizi ya Maghazi kama lilifanywa kwa makosa. Msemaji wa serikali ya Israel Eylon Levy amesema shambulio hilo limefanyika kimakosa na kwamba Israel inasikitika.

Amesema jambo kama hilo halikupaswa kutokea. lakini limefanyika kutokana na uchaguzi wa silaha zilizotumika usiokuwa sahihi.

Wakati hayo yakiendelea Misri inatazamiwa kuwa mwenyeji wa mazungumzo nawajumbe wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas kuhusu kusitisha vita kati ya Israel na Hamas ambavyo vimesababisha uharibifu mkubwa katika Ukanda wa Gaza.

Mkutano huo wa mjini Cairo unafanyika wakati mapigano yanaendelea kupamba moto katika maeneo ya kusini na katikati mwa mji wa Gaza uliozingirwa.

UN: watu zaidi ya laki moja wawasili katika mji wa Rafah

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu imesema watu wengine wapatao 100,000 waliokimbia makaazi yao wamewasili katika mji wa mpakani wa kusini wa Rafah katika siku za hivi karibuni kutokana na kuongezeka kwa mapigano karibu na miji ya Deir al-Balah na Khan Yunis.

Msafara mwingine wa malori ya misaada waingia Gaza

Huko nchini Israel vyombo vya habari vimeripoti kwamba watu nchini humo wamekuwa wakiandamana mara kwa mara kuipinga serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, wanayoilaumu kwa kutofanya vya kutosha ili kuwezesha kuachiliwa kwa mateka wa Israel waliobaki mikononi mwa Hamas.

Wakati huo huo Pakistan imepiga marufuku sherehe za mkesha wa mwaka mpya ili kuonyesha mshikamano na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Soma pia:Idadi ya waliofariki Gaza yaongezeka baada ya mapigano kuanza tena

Katika hotuba yake kwa taifa, Waziri Mkuu Anwaar-ul-Haq Kakar amesema, kwa sababu ya hali katika Ukanda wa Gaza, serikali yake imepiga marufuku kila aina ya matukio kuhusu sherehe za Mwaka Mpya.

Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi kadhaa za magharibi zimeliorodhesha kundi la Hamas kama kundi la kigaidi.