1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAfghanistan

Mataifa yajadili haki za wanawake wa Afghanistan

2 Mei 2023

Wawakilishi wa mataifa kadhaa pamoja na taasisi za kimataifa wamekutana Qatar kwa mazungumzo yaliyojikita kuangazia masuala yahusuyo haki za wanawake nchini Afghanistan chini ya utawala wa Taliban.

https://p.dw.com/p/4Qn3C
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia mkutano unaojadili haki za wanawake nchini Afghanistan, unaofanyika mjini Doha.
Umoja wa Mataifa umejikuta katika njia panda ya ama kuendelea kuisaidia Afghanistan ama la kufuatia hatua zake dhidi ya wanawake.Picha: Karim Jaafar/AFP/Getty Images

Hata hivyo serikali ya Taliban haikuwakilishwa katika mkutano wa ndani unaofanyika kwa siku mbili na yaliyoanza jana Jumatatu yanayoratibiwa na Umoja wa Mataifa. 

Wajumbe kutoka Marekani, Urusi, China na wengine kutoka mataifa 20 pamoja na mashirika makubwa ya misaada kutoka barani Ulaya, na jirani yake Pakistan waliungana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwenye mazungumzo hayo ya mjini Doha, ambayo kulingana na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, hayatagusia lolote kuhusu kuitambua rasmi serikali ya Taliban. Makundi ya utetezi wa haki za binaadamu nchini humo yanahofia huenda suala hilo likajadiliwa.

Amesema akiwa makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kwamba, wajumbe hao wanalenga kuwa na makubaliano ya pamoja katika masuala muhimu kuhusu haki za binaadamu na hasa kwa wanawake na wasichana, utawala shirikishi, kupambana na ugaidi na biashara ya dawa za kulevya.

Mamlaka za Taliban zimeanzisha msururu wa sheria kali, tangu serikali iliyoungwa mkono kimataifa ilipoondoka Agosti mwaka 2021, ambazo Umoja wa Mataifa inaziita ni za ubaguzi wa kijinsia. Sheria hizo ni pamoja na zinazowazuia wanawake kujiunga na karibu vyuo vyote vikuu pamoja na elimu ya sekondari na hata kuajiriwa serikalini. Mwezi uliopita tu, mamlaka za Taliban zililiongeza muda wa zuio kwa wanawake kufanya kazi kwenye taasisi za kimataifa.

Soma Zaidi: UN kufanya mazungumzo na Taliban kuhusu wanawake

 

Wanafunzi wanawake wa chuo kikuu wakiwa amesimama mbele ya mlinzi katika lango la chuo kikuu cha Taliban Disemba 21, 2022, kufuatia zuio la serikali kwa wanawake kujiunga a vyuo vikuu.
Haki za wanwake nchini Afghanistan zimekuwa zikizuiwa vibaya tangu serikali ya Taliban ilipoingia madarakabi mwaka 2021. Picha: Wakil Kohsar/AFP/Getty Images

Taliban yonya masuala yake ya ndani kutotumika kama siaha dhidi yake.

Taliban yenyewe inasema zuio hilo ni suala la ndani ambalo halipaswi kuathiri kwa namna yoyote mahusiano ya kimataifa.Na hata siku ya jana Taliban kupitia naibu msemaji wake Bilal Karimi, kwa mara nyingine ilionya juu ya suala hilo kutumika kama silaha ya kisiasa dhidi yao na kusisitiza kwamba wanataka ushirikiano mzuri na mataifa yote ulimwenguni.

"Hapana shaka kwamba Afghanistan iko tayari kuwa na maingiliano mazuri na jumuiya ya kimataifa, lakini jambo moja tunalopaswa kuweka wazi ni kwamba masuala ya kijamii na masuala ya ndani ya watu wa Afghanistan hayapaswi kutumiwa kama zana za kisiasa," alisema Karimi.

Umoja wa Mataifa umesema unakabiliwa na wakati mgumu wa kuchagua, linapokuja suala la kuendeleza juhudi zake za kuisidia Afghanistan, na Guterres anatarajiwa kutoa tamko kuhusu hatua zilizofikiwa kuhusiana na suala hilo baada ya mapitio yatakayokamilika siku ya Ijumaa.

Soma Zaidi: Umoja wa Mataifa waangazia kusitisha shuguli zao Afghanistan

Hata hivyo, mwanadiplomasia mmoja anayeshughulikia Afghanistan amesema kusitarajiwe lolote kubwa kutoka Doha, ingawa  hali inaweza kubadilika ikiwa nchi tofauti zitakubali kuchukua majukumu tofauti ya kuiwekea shinikizo kwa Kabul.

Hatimaye waziri wa mambo ya nje wa Taliban afunguliwa milango.

Huku hayo yakiendelea, kamati ya Baraza la Usalama la umoja huo limemruhusu waziri wa mambo ya nje wa Taliban Amir Khan Muttaqi kwenda Pakistan wiki ijayo kukutana na mawaziri wa Pakistan na China, duru za kidiplomasia zimesema. Muttaqi amekuwa akikabiliwa na vizuizi vya kusafiri, mali zake kuzuiwa na vizuizi vya silaha chini ya vikwazo vya baraza hilo.

Kulingana na barua kwa wanachama 15 wa baraza hilo, Kamati ya vikwazo vya Taliban na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Pakistan waliomba kuondolewa kwa kizuizi cha kusafiri kati ya Mei 6-9 ili kukutana na mawaziri wa mambo ya nje wa Pakistan na China. Barua hiyo hata hivyo haikusema kitakachojadiliwa na mawaziri hao