1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMali

Mataifa ya ukanda wa Sahel yanahangaishwa na uasi

12 Januari 2023

Ni miaka 10 tangu majeshi ya Ufaransa yalipoongoza mashambulizi katika mji wa Konna huko Mopti ili kuzuia kusonga mbele kwa makundi ya kigaidi kuelekea mji mkuu wa Mali.

https://p.dw.com/p/4M5SV
Mali | Militär | FAMA | Armed forces
Picha: Souleymane Ag Anara/AFP

Mnamo Januari 2013 kufuatia ombi la mamlaka ya mpito ya Mali iliyoongozwa wakati huo na Dioncounda Traoré, jeshi la anga la Ufaransa lilifanya mashambulio katika eneo hilo la katikati mwa Mali.

soma EU itakuwa na ushiriki gani kiusalama nchini Mali, 2023?

Ilianza kama Operesheni Serval, ambayo baadaye ilibadilika na kuwa operesheni Barkhane. Miaka 10 baadaye, hali bado ni tete na hakuna mwanajeshi wa Ufaransa aliye kwenye eneo la Mali baada ya kusitishwa kwa ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili mnamo Mei 2022.

soma Mali na Ivory Coast zajaribu kutatua mivutano yao

Katika matukio ya hivi karibuni jeshi la Mali limesema kwamba wanajeshi wake 14 waliuawa na wengine 11 kujeruhiwa katika mapigano dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu wiki hii.

Mapigano yalizuka wakati kikosi cha jeshi kiliposhambuliwa kwa mabomu kando ya barabara kati ya miji ya Mopti na Segou katikati mwa Mali.

Siku ya Jumatano, maafisa wa jeshi na polisi, walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina, walisema wanajeshi wasiopungua 12 walikufa.

Mali iko katika lindi la mgogoro wa kiusalama uliodumu kwa takriban miaka 11 uliosababishwa na uasi wa eneo la kaskazini ambao uliibuka na kuwa uasi kamili wa wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu.

Maelfu ya watu wamekufa na mamia ya maelfu wamekimbia makaazi yao, na ukosefu wa maridhiano ndani ya jeshi ulichochea mapinduzi mnamo Agosti 2020.

Mfulilizo wa mapinduzi ya kijeshi

Burkina Faso | Armee Putschisten Traore
Jeshi la Burkina FasoPicha: Kilaye Bationo/AP/dpa/picture alliance

Uasi huo ulienea hadi nchi jirani za Niger na Burkina Faso mwaka 2015, na kufuatiwa na mashambulizi ya hapa na pale katika nchi za kusini, kando ya Ghuba ya Guinea.

Huku haya yakijiri serikali ya Burkina Faso imesema kwamba, Mkuu wa kanda ya Afrika Magharibi ameiunga mkono Burkina Faso, chini ya miezi mitano baada ya uasi uliochochewa na wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu na kuzusha mapinduzi mapya.

Rais wa Guinea Bissau Umaro Sissoco Embalo, ambaye pia ni rais wa sasa wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), alifanya ziara ya siku moja mjini Ouagadougou siku ya Jumatano kwa mazungumzo na kiongozi wa jeshi Kapteni Ibrahim Traore.

soma Ibrahim Traore kuapishwa Ijumaa kama rais wa mpito

ECOWAS, jumuiya yenye wanachama 15 inapambana na mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi katika eneo lake na kuongezeka kwa uasi wa wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislam katika ukanda wa Sahel.

Maelfu ya watu wamefariki dunia na zaidi ya watu milioni mbili wamekimbia makazi yao tangu wanamgambo hao walipoanza kushambulia Burkina Faso kutoka nchi jirani ya Mali mwaka 2015. Zaidi ya theluthi moja ya maeneo ya nchi hiyo yako nje ya udhibiti wa serikali.

 

//AFP