1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUrusi

BRICS yaanda mkutano kujadili kadhia ya vita nchini Ukraine

10 Septemba 2024

Wawakilishi wa kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani BRICS wanatarajiwa kujadili juu ya vita vinavyoendelea nchini Ukraine katika mkutano wa usalama ulioanza leo Jumanne.

https://p.dw.com/p/4kSbl
Südafrika Johannesburg | Narendra Modi und Cyril Ramaphosa beim bilateralen Treffen auf dem 15. BRICS-Gipfel
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wakiongoza ujumbe wa nchi hizo mbili kwenye mkutano wa BRICS uliofanyika Afrika Kusini mwezi Agosti mwaka 2023Picha: Naveen Jora/ZUMA Press/picture alliance

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema anataraji kuwa kiongozi wa China Xi Jinping atahudhuria mkutano wa kilele wa kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani BRICS utakaofanyika nchini Urusi mwezi ujao. Urusi pia imemualika mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman kuhudhuria mkutano huo.

Rais Putin ameeleza wakati wa mkutano na makamu wa rais wa China Han Zheng pembezoni mwa jukwaa la kiuchumi la mashariki lililofanyika mjini Vladivostok kuwa, anataraji kiongozi wa China Xi Jinping atahudhuria mkutano wa kilele wa BRICS.

Soma pia: India, China na Brazil zaweza kuwa wapatanishi, asema Putin

Putin amekuwa akimtegemea kiongozi huyo wa China tangu kuzuka kwa mzozo kati ya Urusi na Ukraine, huku nchi hizo mbili, China na Urusi, zikiimarisha ushirikiano wa kibiashara wakati Moscow ikikabiliwa na vikwazo vya kiuchumi kutoka mataifa ya Magharibi.

Urusi kutumia mkutano wa BRICS kutanua ushawishi wake

Urusi| St. Petersburg 2024 | Putin akifanya mkutano na spika wa bunge
Rais wa Urusi Vladimir Putin akifanya mkutano na baadhi ya viongozi wa serikali yake akiwemo spika Valentina MatviyenkoPicha: Valery Sharifulin/POOL/dpa/picture alliance

Kundi la mataifa ya BRICS yanayojumuisha Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini, yanawakilisha karibu nusu ya idadi jumla ya watu duniani kote na sasa kundi hilo limepanuka na kujumuisha mataifa mengine yanayoinukia kiuchumi ikiwa ni pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu na Iran.

Kundi hilo la BRICS linatarajiwa kufanya mkutano wa kilele mjini Kazan, Urusi kuanzia Oktoba 22 hadi 24 katika kile ambacho Kremlin inaeleza kuwa mkutano huo utakuwa fursa adhimu ya kutanua ushawishi wake na pia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na mataifa mengine.

China na Urusi, zote zinapinga kile kinachojulikana kama "ubabe wa Magharibi" hasa udhibiti wa Marekani katika mfumo wa kimataifa. Moscow na Beijing pia zilitangaza ushirikiano wa "bila mipaka" muda mfupi tu kabla ya Urusi kuivamia Ukraine.

Soma pia: Serbia yamuahidi Putin kwamba kamwe haitaigeuzia mgongo

Mwezi uliopita, wakati Putin alipokuwa akimkaribisha Waziri Mkuu wa China Li Qiang katika ikulu ya Kremlin, kiongozi huyo wa Urusi aliweka wazi kwamba uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Urusi unaendelea kupata matokeo chanya.

Wakati huo huo, Urusi imemualika mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman katika mkutano huo wa BRICS.

Kundi la BRICS liliialika Saudi Arabia, Iran, Ethiopia, Misri, Argentina na Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa wanachama, katika hatua ambayo inalenga kubadilisha mfumo wa kimataifa wa dunia ambao wanauona kama uliopitwa na wakati.

Vyanzo viwili vilivyo na ufahamu juu ya suala hilo vimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba Saudi Arabia bado inafikiria juu ya mwaliko wa kujiunga rasmi na kundi la BRICS.

Putin ashinda uchaguzi wa rais

Wakati hayo yanaarifiwa, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa imeuteka mji wa Krasnogorivka ulioko mashariki mwa Ukraine pamoja na vijiji vitatu katika maeneo tofauti ya mkoa wa Donetsk.

Wizara hiyo imeendelea kueleza kuwa, wanajeshi wa Urusi wameukomboa mji huo pamoja na vijiji vya Grygorivka, Galytsynivka na Vodiane.

Soma pia: Watu 41 wauawa katika mashambulio ya Urusi nchini Ukraine

Wizara hiyo imetumia majina ya Kirusi kutambulisha maeneo hayo yaliyoiteka.

Wanajeshi wa Urusi wamekuwa wakisonga mbele katika mkoa wa Donetsk katika wiki za hivi karibuni na wanakaribia kufika mji wa Pokrosk, kitovu muhimu cha usafirishaji wa vifaa kwa vikosi vya Ukraine.

Wiki iliyopita, Rais Vladimir Putin alisema kuuteka mkoa wa Donbas, mji wa kiviwanda wa Ukraine, ni lengo kuu la Urusi.