1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marufuku ya kusafiri yawekwa Italia

10 Machi 2020

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte ametangaza usitishwaji wa matamasha yote ya michezo na ligi ya soka ya nchi hiyo, hatua imbayo imechukuliwa baada ya nyingine kama hiyo ya kuwazuia kusafiri.

https://p.dw.com/p/3Z8Og
Italien Coronavirus
Picha: picture-alliance/AA/P.M. Tacca

Michezo katika ligi ya juu ya nchi hiyo Serie A pamoja na matukio mengine vitasitishwa hadi  Aprili 3 wakati  nchi  hiyo  ikipambana  na kusambaa  kwa  virusi  vya  Corona. Kabla ya serikali kutangaza hatua hiyo, timu ya Sassuolo iliichapa Brescia mabao 3-0 katika mnyukano ambao ulifanyika pasipo kuhudhuria na mashabiki wa soka katika uwanja wa Reggio Emilia hapo jana.

Ujumbe muhimu kwa mchezaji Francesco Caputo.

Baada ya kufunga goli la kwanza mshambuliaji wa Sassuolo, Francesco Caputo alionesha karatasi iliyoandikwa, ikiwa ujumbe wake kwa mashabiki uliosema "Kila kitu kitakuwa sawa, bakini nyumbani." Masaa machache baadae waziri mkuu alitumia maneno hayo hayo wakati akitangaza marufuku ya mikusanyiko na kusafiri kiholela katika kukabiliana na kasi ya virusi vya corona. "Ni wakati sahihi kubaki majumbani. Hatma yetu, hatma ya Italia ipo mikononi mwetu. Na mikono yetu inapaswa kuwa mikono yenye kuwajibika kwa sasa kuliko ilivyokuwa awali. Kila mmoja anapaswa kuchukua nafasi yake. Na hii ndio sababu amri hii inapaswa kutekelezwa katika maeneo yote, siku chache zilizopita tuliweka marufuku katika maeneo ya kaskazini ya Lombardy na majimbo mengine.  Vilevile tumechukua hatua katika maeneo ya michezo. Hapa tulipofikia, na katika muhtadha huu, tunaona hakuna sababu ya kuendelea na matamasha ya michezo."

Idadi ya maambukizi yaongezeka kwa kasi.

Italien Seria A Geisterspiel Coronavirus Parma vs Spal
Ligi ya Seria A ya Italia ikifanyika bila ya mashabikiPicha: picture-alliance/Zuma/P. Cruciatti

Italia ina jumla ya watu 9,172 walioambukizwa virusi vya corona, ikijumuishwa jumla ya visa 1,807 vilivyobainika ndani ya kipindi cha masaa 24. Vifo vilivyotokana na kadhia hiyo pia vimeongezeka kutoka watu 87 hadi kufukia 463 vingi vya vifo hivyo vimewafika wazee. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO watu ambao hawajaathiriwa sana wanaweza kupata unafuu katika kipindi cha wiki mbili, wakati wale ambao wameshambuliwa vibaya wanaweza kufikisha hadi wiki sita.

Wakati kila taifa likifanya jitihda za kukabiliana na virusi hivyo, Israel inawaweka Karantini kwa siku 14 watu wote wanaoingia nchini humo kutoka katika mataifa ya kigeni.

Huko China Bara ambako mrupuko wa virusi vya corona unatajwa kuanzia, zaidi ya watu elfu 80 walibainika kuwa na virusi na zaidi ya watu elfu 58 hadi sasa wamepoma. Na kutokana na hali hiyo Rais Xi Jinping leo ametembelea eneo ambalo linatajwa kama kiini cha virusi vya Corona la mji wa Wuhan, vilikozuka Desemba. Ziara yake inafanyika katika kipindi ambacho maisha katika eneo hilo yanaanza kurejea katika hali ya kawaida na watu kurejea makazini.

APE/APTN