1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya virusi vya Corona Ujerumani yapindukia 1000

Sylvia Mwehozi
9 Machi 2020

Nchini Ujerumani visa vya maambukizi vimepindukia 1000, huku Italia ikiufungia mji wa Lombardy na majimbo kadhaa yaliyoko kaskazini mwa nchi. China bara imeripoti idadi ndogo ya maambukizi tangu mwezi Januari.

https://p.dw.com/p/3Z52p
Deutschland Coronavirus Maßnahmen in Essen
Picha: Reuters/W. Rattay

Nchini Ujerumani visa vya maambukizi vimepindukia 1000, kwa mujibu wa data za taasisi ya udhibiti wa magonjwa Robert Koch. Eneo lililoathirika zaidi Ujerumanini jimbo la North Rhine Westfalia ambalo lina wakaazi wengi.  Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn amesema wametangaza hatua za kuimarisha uchumi unaonekana kutetereka kutokana na kuenea kwa mripuko wa virusi vya Corona wakati pia wakiyazuia matukio yote makubwa yaliyopangwa kufanyika.

Wiki iliyopita maonyesho kadhaa yaliahirishwa ikiwemo maonyesho ya Utalii ya Berlin ITB, maonyesha ya viwanda ya Hannover na yale ya vitabu ya mjini Leipizig. Lakini kutokana na tangazo la hivi sasa, kuna uwezekano hata mechi za Bundesliga nazo zikaahirishwa.

Siku ya Jumapili waziri mkuu wa Italia Giusseppe Conte alisema hatua hizo za kufunga miji, zimeanza mara moja na zitadumu hadi Aprili 3. Hadi Jumapili shirika la ulinzi wa kiraia Italia limesema visa vipya nchini humo vimepanda kwa robo tatu na hadi watu 7,375 na vifo kufikia 366.

Marufuku ya kusafiri imeanza kutumika ndani na nje ya mkoa wa Kaskazini wa Lombardy ikiwemo mji wa kibiashara wa Milan ambao umeathiriwa mno na virusi hivyo. Watalii ambao hivi sasa wamo katika maeneo yaliyoathirika, ambayo pia yanajumuisha majimbo mingine 14 ya kaskazini, yakiwemo Venice na Parma, wataruhusiwa kuondoka kwa haraka, amesema Conte.

"Baraza la mawaziri limechukua hatua kadhaa; tumetenga euro 7.5 bilioni kuzisaidia familia na wafanyabiashara walio na dharura, ambayo tumesema sio tu ni dhahura ya kiafya pia ni ya kiuchumi," alisema waziri mkuu Conte.

Coronavirus - Italien - Leere Stühle vor Café
Mgahawa ukiwa wazi mjini Venece baada ya tangazo la mpango wa dharuraPicha: picture-alliance/G. Cosua

Wakati huo China Bara, nje kidogo ya jimbo la Hubei, hakuna visa vipya vya maambukizi ya ndani vilivyoripotiwa kwa siku ya pili mfululizo, lakini katibu mkuu wa chama cha kikomonisti ameonya kwamba hawapaswi kupunguza hadhari dhidi ya mripuko huo. Hadi jana visa vipya vya maambukizi nchini China vilikuwa 40 lakini vikiwa vimeshuka toka 44 siku moja iliyopita na ikiwa pia ni idadi ndogo tangu mamlaka za afya zilipoanza kutoa takwimu nchi nzima Januari 20.

Vyanzo: Reuters/AFP/DPA